

Lugha Nyingine
Kenya yawasilisha rasmi uteuzi wa Odinga kugombea mwenyekiti wa Kamati ya AU
NAIROBI - Kenya imewasilisha rasmi uteuzi wa Raila Odinga, kiongozi mkongwe wa upinzani na waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, kugombea mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika (AUC) katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 2025, Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje wa Kenya Korir Sing'Oei amesema siku ya Jumatatu.
Sing'Oei amesema amewasilisha ombi la Odinga kwa Mkuu wa Kanda ya Mashariki Dharmraj Busgeeth, ambaye pia ni balozi wa Mauritius.
"Chini ya mamlaka ya Serikali ya Kenya na kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Kamati ya Umoja wa Afrika, leo tumewasilisha rasmi nyaraka zinazohitajika za mteule wa Kenya kwa mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika," Sing'Oei amesema.
Kiti cha mwenyekiti wa AUC kinatarajiwa kuwa wazi mwezi wa Februari Mwaka 2025 kwani mwenyeji wake wa sasa kutoka Chad, Moussa Faki atamaliza muhula wake wa pili.
Faki aliteuliwa kwa mara ya kwanza Mwaka 2017 na alishinda muhula wa pili Mwaka 2021.
Mwenyekiti wa AUC huchaguliwa na Baraza Kuu la Wakuu wa Nchi na Serikali za Bara la Afrika kwa muhula wa miaka minne, unaoweza kuongezwa mara moja.
Kwa mujibu wa kanuni ya mzunguko miongoni mwa kanda zinazounda Bara la Afrika, sasa ni zamu ya kanda ya Afrika Mashariki kuwasilisha wagombea wa nafasi ya mwenyekiti.
Odinga ambaye amewahi kuwania kiti cha urais nchini Kenya kwa mara tano bila mafanikio, anatarajiwa kuwania nafasi hiyo dhidi ya wagombea watatu kutoka kanda ya Afrika Mashariki akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahmoud Youssouf, Naibu Waziri Mkuu wa zamani na mbunge wa sasa wa Bunge la Somalia, Fawzia Yusuf na Makamu Rais wa zamani wa Ushelisheli, Vincent Meritoni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma