Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika 2024 kufanyika Beijing Septemba 4 hadi 6

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 31, 2024

BEIJING - Mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) Mwaka 2024 utafanyika Beijing kuanzia Septemba 4 hadi 6, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Hua Chunying ametangaza siku ya Jumanne.

Hua amesema, Kaulimbiu ya mkutano huo ni "Kushikamana Kuhimiza Ujenzi wa Mambo ya Kisasa na Kujenga Jumuiya ya Kiwango cha Juu ya China na Afrika yenye Mustakabali wa Pamoja," na viongozi wa Afrika washiriki wa FOCAC watahudhuria mkutano huo kwa mwaliko kutoka kwenye baraza hilo.

“Wawakilishi wa mashirika husika ya kikanda ya Afrika na mashirika ya kimataifa watashiriki kwenye shughuli husika za baraza hilo,” ameongeza.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika siku hiyo ya Jumanne, msemaji mwingine wa wizara hiyo Lin Jian amesema mkutano huo wa FOCAC mwaka huu utakuwa ni mkutano wa kilele wa mara ya nne wa baraza hilo, ambapo pande hizo mbili kwa pamoja zitazungumza kuhusu urafiki, ushirikiano na hali ya siku za baadaye.

Lin amesema mikutano ya maofisa wa ngazi za juu na mawaziri itafanyika Septemba 2 na 3, mtawalia, ili kufanya maandalizi ya mkutano huo wa kilele. Kuanzia Septemba 4 hadi 6, shughuli mbalimbali mfululizo zitafanyika ikiwa ni pamoja na hafla ya ufunguzi wa mkutano, karamu ya makaribisho, maonyesho ya michezo ya Sanaa, mikutano sambamba ya ngazi ya juu, mkutano wa wajasiriamali wa China na Afrika na mikutano ya pande mbilimbili.

“Hii ni mara ya pili kwa familia ya China na Afrika kukusanyika mjini Beijing kufuatia Mkutano wa kilele wa FOCAC wa Mwaka 2018,” amesema Lin.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha