

Lugha Nyingine
Rais wa zamani Zuma afukuzwa chama tawala cha Afrika Kusini, ANC
Jacob Zuma akishiriki kwenye kampeni ya Chama cha Umkhonto weSizwe (MK) mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Mei 18, 2024. (Picha na Ihsaan Haffejee/Xinhua)
JOHANNESBURG - Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini kimethibitisha kuwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma, amefukuzwa uanachama wa chama hicho baada ya kukiuka katiba ambapo Fikile Mbalula, Katibu Mkuu wa ANC ametangaza kuwa Kamati ya Kitaifa ya Nidhamu ya ANC imemkuta Zuma na hatia ya kukiuka katiba kwa kuathiri hadhi ya chama kupitia "kufanya kazi kwa ushirikiano na chama kingine cha kisiasa kilichosajiliwa."
"Mwanachama aliyeshtakiwa anafukuzwa kutoka ANC," amesema Mbalula kwenye makao makuu ya chama hicho mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Mbalula ameongeza kuwa Zuma anaweza kukata rufaa ya kufukuzwa kwake ndani ya siku 21.
Suala hilo lilianza Desemba mwaka jana wakati Zuma alipotangaza kwamba ataunga mkono Chama kipya cha Umkhonto weSizwe (MK) kwenye uchaguzi mkuu wa Mei 2024. ANC ilisimamisha uanachama wa Zuma mwezi Januari mwaka huu na kupeleka mashtaka dhidi yake kwenye kamati ya nidhamu.
Kuanzishwa kwa Chama cha MK, ambacho kilipata asilimia zaidi ya 14 ya kura katika uchaguzi huo, kulisababisha ANC kupoteza wingi wa viti vyake bungeni kwa mara ya kwanza tangu Mwaka 1994.
Zuma alikua Rais wa ANC Mwaka 2007 kufuatia mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho na baadaye alichaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini kuanzia Mwaka 2009 hadi 2018 alipoondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye kabla ya kumaliza muhula wake.
Julai 2021, Zuma alifungwa jela kwa kosa la kudharau mahakama baada ya kushindwa kutii amri ya mahakama ya kufika mbele ya kamati teule ya uchunguzi wa serikali kuwekwa mfukoni na mafisadi, ambayo ulichunguza kuenea kwa rushwa na ufisadi uliotokea wakati wa utawala wake.
Chama cha MK kimelalamikia jinsi mchakato wa kinidhamu dhidi ya Zuma ulivyoendeshwa, kikiulinganisha na "mahakama ya kangaroo." Kimeongeza kuwa Zuma atashauriana na wanasheria wake kuhusu hatua inayofuata atakayochukua.
Jacob Zuma akishiriki kwenye kampeni ya Chama cha Umkhonto weSizwe (MK) mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Mei 18, 2024. (Picha na Ihsaan Haffejee/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma