

Lugha Nyingine
China yapaa juu kwenye idadi ya medali huku ikipata medali ya dhahabu ya kihistoria kwenye mchezo wa BMX
Deng Yawen wa China akishindana kwenye fainali ya mchezo wa kuendesha baiskeli kwa mtindo huru, BMX kwa wanawake kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris, Julai 31, 2024. (Xinhua/Hu Huhu)
PARIS - Deng Yawen mwenye umri wa miaka 18, ameshinda medali ya dhahabu ya olimpiki ya kwanza kabisa kwa China katika mchezo wa kuendesha baiskeli kwa mtindo huru, BMX kwa wanawake mjini Paris 2024, huku muogeleaji wa China Pan Zhanle akivunja rekodi ya Dunia kufuatia kushinda taji la mbio za kuogelea kwa mtindo huru za mita 100 kwa wanaume kwa muda wa sekunde 46.40 na kuifanya China hadi sasa kuongoza kwenye orodha ya medali ikiwa na medali tisa za dhahabu, ikifuatiwa na wenyeji Ufaransa na Japan, zote zikiwa na medali nane za dhahabu.
Mwendesha baiskeli huyo wa China Deng alimaliza wa pili katika mashindano ya mchujo siku ya Jumanne, nyuma ya bingwa mara tano wa dunia Hannah Roberts wa Marekani, na ameonyesha kujiamini kwenye jukwaa la Olimpiki.
Deng amepata alama mbili za juu zaidi katika fainali na kunyakua medali hiyo ya dhahabu ya kihistoria, huku Roberts akishika nafasi ya nane baada ya kuanguka.
Pan Zhanle wa China akishindana kwenye fainali ya mbio za kuogelea kwa mtindo huru za mita 100 kwa wanaume katika Michezo ya Olimpiki ya Paris, Julai 31, 2024. (Xinhua/Xue Yuge)
Kwingineko, Pan mwenye umri wa miaka 19 amenyakua medali ya kwanza ya dhahabu kwa China katika mchezo wa kuogelea kwenye Michezo hiyo, akiongoza katika mchakato mzima kupunguza rekodi yake ya dunia ya mita 100 ya kuogelea kwa mtindo huru ya muda wa 46.80 aliyoiweka kwenye Mashindano ya Dunia ya Kuogelea Mwaka 2024 huko Doha.
"Sikutarajia kuvunja rekodi ya dunia kabla ya mbio, nilipanga kuwa na mwanzo imara, najua kuna matumaini makubwa juu yangu, na hatimaye, nimefanya," Pan amesema baada ya kumaliza mashindano.
Mshikaji wa rekodi ya dunia Sarah Sjostrom wa Sweden amewashinda wapinzani wake kunyakua medali ya dhahabu katika mbio za kuogelea kwa mtindo huru za mita 100 kwa wanawake.
Chen Yuxi/Quan Hongchan (mbele) wa China wakishindana kwenye fainali ya wanawake wawili kupiga mbizi pamoja kutoka kwenye jukwaa la kimo cha mita 10 katika Michezo ya Olimpiki ya Paris, Julai 31, 2024. (Xinhua/Li Ying)
Wapiga mbizi wa China wameendelea na mbio zao za dhahabu, huku Chen Yuxi na Quan Hongchan, ambao wameungana na kushinda Mashindano ya Dunia mara tatu mfululizo, wametawala mchezo wa wanawake wawili kupiga mbizi pamoja kutoka kwenye jukwaa la kimo cha mita 10 huko Paris 2024 kwa pointi 359.10, 43.2 wakifuatiwa nawapiga mbizi kutoka DPRK Kim Mi -rae na Jo Jin-mi.
Ushindi huo wa Chen/Quan unamaanisha medali ya dhahabu ya 7 mfululizo ya Olimpiki kwa China katika mchezo huu na medali ya tatu ya dhahabu kwa timu hii huko Michezo ya Olimpiki ya Paris.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma