

Lugha Nyingine
China yahimiza juhudi za kuzuia mafuriko wakati ambapo mvua zinaendelea kunyesha
Wafanyakazi wa uokoaji wakifanya oparesheni ya uokoaji katika Mji wa Linjiang, Mkoa wa Jilin, Kaskazini Mashariki mwa China, Julai 29, 2024. (Xinhua/Zhang Nan)
BEIJING - Wizara ya Usimamizi wa Dharura ya China imetoa wito siku ya Jumapili kwa mamlaka mbalimbali husika kuwa macho dhidi ya mafuriko kwani mvua kubwa inatabiriwa kuendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo ya China katika siku zijazo.
Wizara hiyo imesema kuwa, ingawa jumla ya mvua nchini humo itapungua kwa muda katika siku tatu zijazo, mvua inayoweza kupimika bado inakadiriwa kunyesha katika eneo la kaskazini-mashariki, mabonde ya Mto Manjano na Mto Huaihe, na Mkoa wa Yunnan, Kusini-Magharibi mwa China.
Kazi ya kuzuia mafuriko bado inakabiliwa na changamoto, imesema wizara hiyo, huku ikibainisha kuwa viwango vya maji vinaendelea kuwa juu ya alama za tahadhari katika Mto Liaohe na sehemu ya Mto Songhuajiang, ambayo yote iko kaskazini mashariki mwa China.
“Idara na sekta mbalimbali husika zinapaswa kutimiza wajibu wao, kushinda ulegevu na uchovu, na kuendelea kukagua na kulinda sehemu hatarishi za kingo za mito,” kwa mujibu wa wizara.
Imehimiza kuwa ni lazima kuwa na macho dhidi ya maafa yanayosababishwa na mvua kubwa na mafuriko, ikiagiza usimamizi thabiti wa usalama wa maeneo ya vivutio vya watalii ya baharini na barabara kuu karibu na miteremko ya milima na miamba. Imetoa wito kwa wafanyakazi husika kujifunza kutokana na matukio ya sehemu husika, kama vile kuporomoka kwa barabara na madaraja ambako kumesababisha vifo na majeraha ya watu.
Watu wanne walikuwa wamefariki dunia na wengine 23 walikuwa hawajulikani walipo hadi kufikia saa 5 usiku Jumamosi baada ya mafuriko na maporomoko makubwa ya matope kupiga mji wa Kangding Mkoa wa Sichuan, kusini-magharibi mwa China kutokea saa 9:30 alfajiri siku ya Jumamosi, yakiangusha daraja la handaki na kuharibu nyumba katika kijiji kimoja, kwa mujibu wa serikali ya mtaa husika.
Droni kubwa ilikuwa kimetumwa katika eneo lililokumbwa na maafa huko Kangding ili kutoa uungaji mkono wa uchunguzi na mawasiliano, wizara hiyo imesema.
Pamoja na Makao Makuu ya Serikali ya China ya Kuzuia Mafuriko na Kukabiliana na Ukame, wizara hiyo imefanya majadiliano ya pamoja na mamlaka za hali ya hewa, rasilimali maji na maliasili siku ya Jumapili na kupanga kazi ya kuzuia mafuriko katika mikoa muhimu kama vile Mongolia ya Ndani, Liaoning, Jilin, Heilongjiang, Hunan na Sichuan kupitia njia ya video.
Wizara pia imetoa wito wa kuimarishwa kwa kazi ya kuondoa maji na kuzuia milipuko ya magonjwa, na kuharakisha ukarabati wa baada ya maafa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma