Tanzania yaimarisha usimamizi mpakani baada ya ugonjwa wa mpox kuripotiwa katika nchi jirani

(CRI Online) Agosti 05, 2024

Wizara ya Afya ya Tanzania imesema Tanzania imeimarisha usimamizi na udhibiti kwenye vituo vya kuingia na kutoka nchini humo baada ya maambukizi ya mpox kuripotiwa katika nchi jirani za Burundi, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya ya Tanzania Englibert Kayombo amesema siku ya Jumapili kuwa, timu za wafanyakazi wa afya zimetumwa kwenye vituo vya mpakani nchini humo, ili kuimarisha usimamizi na udhibiti dhidi ya maradhi hayo.

Amesema wafanyakazi wa afya wanafanya ukaguzi kwa wale wanaoingia na kutoka nchini humo na kwamba hadi sasa, hakuna mtu yeyote wa Tanzania aliyethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo wa mpox.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jumatatu ilitoa wito kwa nchi zake nane wanachama kuelimisha wananchi wao jinsi ya kujilinda, ili kuzuia kuenea kwa mpox.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha