

Lugha Nyingine
Barabara Kuu za China zapitia mageuzi ya kijani
Vifaa vya kuchaji magari yanayotumia umeme (EV) vikionekana katika eneo la kutoa huduma katika barabara kuu huko Taiyuan, Mkoa wa Shanxi, Kaskazini mwa China, Julai 12, 2024. (Xinhua)
TAIYUAN – Huku idadi inayoongezeka ya vifaa vya nishati safi vikianza kutumika, barabara kuu za China zinapitia mageuzi ya kijani ambapo kando ya barabara kuu inayounganisha miji ya Taiyuan na Xinzhou katika Mkoa wa Shanxi, kaskazini mwa China, paneli za kuzalisha umeme kwa jua (PV) zimejipanga kwenye miteremko na paa, na vifaa vya kuchaji magari yanayotumia nishati ya umeme (EV) vinaonekana kwa kasi ya kuongezeka katika maeneo ya kutoa huduma kwenye barabara kuuna katika vituo vya ulipiaji ushuru wa matumizi ya barabara.
"Miaka kumi iliyopita, vifaa vya kuchaji EV katika maeneo ya kutoa huduma kwenye barabara kuu hizo vilikuwa nadra, lakini sasa ni karibu jambo la kawaida," amesema Liu Xia, ambaye alikuwa akichaji EV yake kwenye barabara kuu.
Mfumo huo wa paneli za kuzalisha umeme kwa jua (PV) wa barabara kuu ulianza kufanya kazi kikamilifu mwezi wa Novemba mwaka jana, na uliidhinishwa kuwa mradi wa kielelezo wa PV wa kiwango cha kitaifa na Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China mwaka huu.
China ni nchi inayoongoza katika sekta ya nishati mbadala duniani, na ni taifa lenye maili ndefu zaidi za barabara kuu duniani. Hadi kufikia mwisho wa Juni, magari milioni 24.72 yanayotumia nishati mpya (NEVs) yanatumika nchini China. Na kuna uwezo mkubwa wa maendeleo katika ufungamanishaji wa barabara kuu na sekta ya PV.
Wizara ya Uchukuzi ya China mapema mwaka huu ilitoa miongozo kuwa, China inahimiza uchunguzi na uanzishwaji wa maeneo ya kutoa huduma kwenye barabara kuu zinazotoa kaboni karibu sifuri, pamoja na ujenzi wa miundombinu husika ya PV.
Maeneo ya ngazi ya mikoa kote China, ikiwa ni pamoja na Shanghai, Sichuan na Hunan, yamezindua mipango ya kuendeleza matumizi ya PV katika maeneo ya barabara kuu, kwa kujikita katika ukubwa na upangaji wa vifaa vya PV, na teknolojia ya kuhifadhi nishati ili kuimarisha utulivu wa mfumo wa nishati na uwezo wa kusimamia usambazaji wa umeme.
Pia katika ajenda ya kitaifa kuna maendeleo ya vifaa na huduma zinazohusiana na aina zingine za nishati safi, kama vile nishati ya hidrojeni.
China imeapa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kufuata njia thabiti ya maendeleo ya kijani na yenye kutoa kaboni chache. Imeahidi kufikia kilele cha utoaji wa hewa ya kaboni kabla ya Mwaka 2030 na kufikia usawazishaji wa utoaji hewa ya kaboni kabla ya Mwaka 2060.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma