Waziri Mkuu wa Ethiopia azindua ujenzi wa eneo la kiuchumi utakaofanywa na kampuni ya China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 15, 2024

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa eneo la kiuchumi utakaofanywa na kampuni ya China mjini Addis Ababa, Ethiopia, Agosti 14, 2024. (Xinhua/Liu Fangqiang)

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa eneo la kiuchumi utakaofanywa na kampuni ya China mjini Addis Ababa, Ethiopia, Agosti 14, 2024. (Xinhua/Liu Fangqiang)

ADDIS ABABA - Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amezindua ujenzi wa eneo la kiuchumi utakaofanywa na kampuni ya China, unaojulikana kama "Eneo Maalum la Kiuchumi la Addis Kesho," katikati mwa Addis Ababa, mji mkuu wa nchi hiyo.

Hafla hiyo ya uzinduzi iliyofanyika Jumatano, imekuja mwaka mmoja baada ya mamlaka ya Jiji la Addis Ababa na Kampuni ya Ujenzi wa Mawasiliano ya China (CCCC) kutia saini mkataba wa eneo hilo la kiuchumi, lenye ukubwa wa hekta 35, kwa gharama inayokadiriwa kufikia dola milioni 700 za Kimarekani.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Abiy amesema eneo hilo la kiuchumi ni sehemu ya dhamira ya serikali ya kuibadilisha Addis Ababa kuwa moja ya miji yenye kuvutia zaidi duniani kwa kujenga jumuia za makazi za kisasa zenye vifaa mbalimbali ikiwemo nyumba za kuishi, maduka makubwa, hoteli na vituo vya starehe.

"Huu ni mwanzo wa ndoto yetu kubwa ya kuifanya Addis Ababa kuvutia kama jina lake 'Ua Jipya' linavyorejelea, na shukrani zangu ziende kwa kampuni ya CCCC na mamlaka ya jiji kwa kuanzisha mradi huu," Abiy amesema.

Kwa mujibu wa waziri mkuu huyo, Eneo Maalum la Kiuchumi la Addis Kesho litaunganishwa na maeneo mengine ya kiuchumi ambayo ujenzi wake unaendelea katika maeneo mengine ya mji mkuu kupitia ujenzi wa ukanda wa Addis Ababa unaoendelea.

Adanech Abiebie, meya wa Addis Ababa, amesema maendeleo ya eneo hilo la kiuchumi ni sehemu ya hatua ya serikali kubadilisha sura ya jiji hilo, kuboresha maisha ya watu, kutoa fursa nyingi za kazi, na kutoa nyumba za kuishi zenye kiwango cha juu.

"Tunachagua CCCC kuwa kampuni ya kujenga mradi huu, tukikubali kwamba ina rekodi ya kufanikiwa kukamilisha miradi mikubwa nchini Ethiopia na nje ya nchi na kuikabidhi kwa wakati na hadi katika ubora wa hali ya juu," Abiebie amesema.

Chen Zhong, naibu meneja mkuu wa CCCC, ameapa kukamilisha na kukabidhi mradi huo kabla ya wakati kwa njia ambayo inaendeleza ushirikiano na mageuzi ya ujuzi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Renato Lu)

Picha