

Lugha Nyingine
China yatangaza majukumu muhimu kwa ajili ya uhifadhi wa ikolojia
Picha ya droni ikionyesha mandhari ya eneo la kivutio cha utalii la Dajinhu la Wilaya ya Taining, Mji wa Sanming, Mkoa wa Fujian, Mashariki mwa China, Agosti 10, 2024. (Xinhua/Jiang Kehong)
FUZHOU – Kamati ya Kitaifa ya Maendeleo na Mageuzi ya China (NDRC), ambayo ni mpangaji mkuu wa uchumi wa nchi hiyo, imetangaza majukumu muhimu siku ya Alhamisi ambayo yatatekelezwa katika kuhifadhi mazingira ya ikolojia.
NDRC itachukua hatua ili kuendeleza mageuzi katika uhifadhi wa ikolojia na kuhimiza maendeleo ya kijani, yanayotoa kaboni chache na ya ubora wa hali ya juu, amesema Zhao Chenxin, naibu mkuu wa kamati hiyo, kwenye shughuli ya kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Ikolojia ya China iliyofanyika katika mji wa Sanming, Mkoa wa Fujian, mashariki mwa China.
Kamati hiyo itafanya kazi kwa bidii, lakini kwa busara, kufikia kilele cha utoaji wa hewa ya kaboni ifikapo Mwaka 2030 na kufikia msawazisho wa utoaji wa hewa ya kaboni ifikapo Mwaka 2060, itaongeza juhudi za kulinda mazingira ya ikolojia, na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo ya kijani na yanayotoa kaboni chache, ameongeza.
NDRC itatekeleza sera za kibajeti, kodi, mambo ya fedha, uwekezaji na za bei, vile vile pamoja na viwango kuunga mkono maendeleo ya kijani na yanayotoa kaboni chache, Zhao amebainisha.
Afisa huyo pia ameahidi kuboresha taratibu za kutimiza thamani ya soko ya bidhaa na huduma za mfumo wa ikolojia, kusukuma mbele fidia jumuishi kwa ajili ya uhifadhi wa ikolojia, na kuboresha utaratibu wa kutoa fidia kwa kuvuka mikoa kwa ajili ya uhifadhi wa ikolojia.
Wakati huo huo, NDRC itaimarisha ushirikiano wa kimataifa kuhusu uchumi wa mzunguko, kuhimiza teknolojia za hali ya juu, bidhaa, viwango na miundo ya biashara kwa ajili ya maendeleo ya kijani na yanayotoa kaboni chache kwenda nchi za nje, na kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa mabadiliko ya tabianchi duniani, Zhao amesema.
Mwaka jana, Bunge la umma la China lilipiga kura kuiteua Agosti 15 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kitaifa ya Ikolojia nchini humo -- kwa lengo la kuongeza uelewa na hatua za umma za kulinda mazingira ya ikolojia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma