Shughuli ya Kumbukumbu za miaka 79 ya kujisalimisha kwa Japan katika Vita vya Pili vya Dunia yafanyika Nanjing, China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 16, 2024

Mwandishi wa habari akipiga picha katika Jumba la Kumbukumbu za Waathiriwa katika Mauaji ya Halaiki ya Nanjing yaliyofanywa na Wavamizi wa Japan huko Nanjing, mji mkuu wa Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China, Septemba 18, 2021. (Xinhua/Li Bo)

Mwandishi wa habari akipiga picha katika Jumba la Kumbukumbu za Waathiriwa katika Mauaji ya Halaiki ya Nanjing yaliyofanywa na Wavamizi wa Japan huko Nanjing, mji mkuu wa Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China, Septemba 18, 2021. (Xinhua/Li Bo)

NANJING - Jumba la Kumbukumbu za Waathirika wa Mauaji ya Halaiki ya Nanjing yaliyofanywa na Wavamizi wa Japan huko Nanjing, mji mkuu wa Mkoa wa Jiangsu, mashariki mwa China siku ya Alhamisi asubuhi limefanya shughuli ya kumbukumbu za miaka 79 tangu Japan ijisalimishe katika Vita vya Pili vya Dunia (WWII).

Agosti 15, 1945, vita vikali vya miaka 14 vya watu wa China kupambana na wavamizi viliisha wakati Japan ilipotangaza kujisalimisha bila masharti.

Watu takriban 30, wakiwemo watoto wa shule, watu wa kujitolea wa vyuo vikuu na vizazi vya watu waliorusurika wa Mauaji ya Halaiki ya Nanjing walishiriki kwenye shughuli hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa maonyesho ambao unaonyesha mandhari iliyoigizwa ya hafla ya kusainiwa vyaraka za kujisalimisha kwa Japan iliyofanyika Nanjing Mwaka 1945.

Wahudhuriaji hao walitazama filamu fupi ya "Countdown to Surrender" kwenye shughuli hiyo.

Ukuta uliojipinda uliojengwa kwa mchanga wa beige umesimama kwenye jumba hilo la maonyesho, ambapo alama 648 za mikono za rangi nyekundu angavu zimewekwa. Alama hizi ni za mikono ya watu wote ambao wana jina moja -- wapiganaji wa Vita vya Watu wa China vya kupambana na Uvamizi wa Japan.

"Hii ni alama ya mkono ya mpiganaji marehemu Zhang Yuhua, ambaye mkono wake wa kulia ulitobolewa kwa risasi wakati wa vita," amesema Zhang Ruochu, mwanafunzi wa darasa la pili mjini Nanjing, akielezea simulizi ya alama za mikono za wapiganaji hao kwa watu walioshiriki kwenye shughuli.

Xia Shuqin ni mtu aliyenusurika wa Mauaji ya Halaiki ya Nanjing. Siku ya Alhamisi asubuhi, mjukuu wake, Xia Yuan, na mjukuu wa kitukuu, Li Yuhan, pia walishiriki kwenye shughuli hiyo. Mwaka 2022, Xia na Li walitambuliwa kuwa warithi wa kumbukumbu za kihistoria kuhusu Mauaji ya Halaiki ya Nanjing.

Mauaji ya Halaiki ya Nanjing yalifanyika wakati wanajeshi wa Japan walipokalia Mji wa Nanjing ambao ulikuwa mji mkuu wa China wa wakati huo, Desemba 13, 1937.

Kwa wiki zaidi ya sita, wavamizi hao waliua raia na askari wasio na silaha wa China takriban 300,000 katika moja ya matukio ya kishenzi ya WWII. Leo, kuna watu 32 tu walionusurika wa mauaji hayo waliojiandikisha waliohai.

Katika mkesha wa siku ya kumbukumbu hiyo ya kujisalimisha kwa Wavamizi wa Japan, askari wa zamani wa Kikosi cha 731 cha Jeshi la Japan, Hideo Shimizu mwenye umri wa miaka 94, alitembelea eneo la zamani la Kikosi cha 731 na Jumba la Maonyesho ya Uhalifu Uliofanywa na Kikosi cha 731 cha Jeshi la Kifalme la Japan huko Harbin, Mkoa wa Heilongjiang, Kaskazini Mashariki mwa China.

Jana, siku ya Alhamisi, Shimizu alimaliza ziara yake ya siku nne ya kuomba msamaha. "Huenda hii ikawa nafasi yangu ya mwisho kuja China kuomba msamaha," amesema Shimizu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha