

Lugha Nyingine
Mtunza Makaburi ya TAZARA alinda kumbukumbu za Mshikamano kati ya China na Tanzania
Saidi, mtunza makaburi, akisafisha makaburi ya Gongo la Mboto huko Dar es Salaam, Tanzania, Agosti 12, 2024. (Picha na Emmanuel Herman/Xinhua)
Kila asubuhi, Msafiri na mwenzake Saidi wanaanza siku yao wakiwa watunza makaburi katika kitongoji cha magharibi mwa Dar es Salaam, wakilinda kumbukumbu ya wahandisi na wafanyakazi wa China waliofariki wakati walipojenga Reli ya TAZARA.
"Nimekuwa nikifanya kazi katika makaburi haya kwa karibu miaka 20 kuhakikisha kuwa sehemu hiyo takatifu inahifadhiwa vizuri ili kuonyesha heshima kwa mashujaa wa China waliopoteza maisha yao," alisema Msafiri Omary, mfanyakazi mwenye umri wa miaka 43 wa Shirika la Ujenzi wa Uhandisi wa Kiraia la China (CCECC) tawi la Afrika Mashariki.
Katika miongo mitano iliyopita, wahandisi, mafundi, na wafanyakazi 70 wa China walipoteza maisha yao wakati walipojenga Reli ya TAZARA na kusaidia maendeleo ya Tanzania. Majina yao yaliandikwa kwenye mawe ya makaburi yao, ambayo yanasimama kimya katika makaburi ya Gongo la Mboto.
Wakati wa kipindi muhimu cha maendeleo ya uchumi wa Tanzania na Zambia katika miaka ya 1970, takriban wafanyakazi na wahandisi wa China 50,000 walifika katika nchi hizo mbili kusaidia kujenga reli ya TAZARA.
Msafiri alisema anajionea fahari kubeba jukumu la kulinda makaburi hayo, kwa sababu majina ya wataalamu wa China yanawakilisha sio tu ushahidi wa kihistoria wa urafiki kati ya China na Afrika, bali pia ni mnara wa kumbukumbu wa uhusiano thabiti na wa kudumu kati ya China na Afrika.
"Wataalamu wa China waliozikwa hapa walijitolea jasho na damu yao hadi tone la mwisho kuhakikisha kuwa reli inakamilika, na ilibaki kumbukumbu isiyofutika inayothibitisha urafiki kati ya China na Tanzania, pamoja na kati ya China na Afrika," alisema Msafiri.
Watunza makaburi Msafiri (kulia) na Saidi wakisafisha makaburi ya Gongo la Mboto huko Dar es Salaam, Tanzania, Agosti 12, 2024. (Picha na Emmanuel Herman/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma