Lugha Nyingine
Mabadilishano na ushirikiano katika nyanja ya lugha kati ya China na Afrika ni muhimu kwa uunganishaji wa mioyo ya watu kati ya pande hizo mbili
Mkutano wa Kilele wa 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) utafanyika kuanzia kesho Jumatano mjini Beijing na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki Dkt. Caroline Asiimwe amesema kuwa, mabadiliano na ushirikiano wa nyanja ya lugha kati ya China na Afrika yanasaidia kuunganisha mawasiliano ya watu kati ya pande hizo mbili.
Asiimwe ameyasema hayo wakati akiwa nchini China kushiriki katika shughuli za vyombo vya habari za “Washirika wa Afrika” kwenye mahojiano na Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG).
Mwaka 2021 Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) uliiteua Julai 7 ya kila mwaka kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani. Kiswahili ikiwa lugha ya kienyeji ya Afrika, mashirika ya kimataifa na wadau wa sekta mbalimbali wanajitahidi kuhimiza umhimu wake katika mawasliano, na hivi sasa Kiswahili kimetambuliwa kuwa lugha muhimu ya kuhimiza mshikamano na amani ya kikanda.
Dkt. Asiimwe amesema amefurahi kuona kuwa China pia inafanya juhudi za dhati za kukuza lugha ya Kiswahili, na kama mwakilishi wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, anaona kuwa shughuli hizo ni mwanzo wa ushirikiano na mabadilishano kati ya CMG na nchi za Afrika katika ushirikiano wa lugha ya Kiswahili.
Wakati huo huo, amesema mbali na ushirikiano kati ya vyombo vya habari, vyuo vikuu vingi vimeanzisha kozi ya lugha ya Kiswahili. Anaamini kuwa mabadilishano na ushirikiano wa nyanja ya lugha na utamaduni ni muhimu sana, kwa kuwa lugha inagusa mioyo ya watu, na utamaduni unahusiana na maisha ya watu.
Mabadilishano na ushirikiano katika nyanja ya lugha kati ya China na Afrika yanasaidia watu wa China na Afrika kuelewana vizuri na kuwafanya kuwa karibu zaidi, na kuhimiza ushirikiano kukita mizizi katika mioyo ya watu wa pande hizo mbili.
Akizungumzia Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika utakaofanyika wiki hii Dkt. Asiimwe anatarajia kuwa mkutano huo utafikia makubaliano zaidi ili kuchangia maendeleo na kunufaisha zaidi watu wa pande hizo mbili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma