Lugha Nyingine
CAEA na IAEA zasaidia Afrika kuwaandaa wataalamu wa fizikia wa tiba ya mionzi
Wahudhuriaji wa mafunzo kutoka nchi za Afrika wakishiriki kwenye programu ya mafunzo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Nishati ya Atomiki ya China (CAEA) na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) wa kuwaandaa wataalamu wa fizikia wa tiba ya mionzi, huko Chengdu, Mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China, Septemba 2, 2024.(CAEA/Kupitia Xinhua)
CHENGDU - Mamlaka ya Nishati ya Atomiki ya China (CAEA) na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) hivi karibuni zimeanza programu ya mafunzo ya kuwaandaa wataalamu wa fizikia wa tiba ya mionzi kwa nchi za Afrika.
Chini ya mpango wa "Miale ya Matumaini" wa IAEA, programu hii ya mafunzo ya miezi mitatu, iliyozinduliwa Chengdu, mji mkuu wa Mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China itatoa mafunzo kwa wataalamu wa fizikia wa tiba ya mionzi kwa ajili ya matibabu ya saratani na uvimbe. Inalenga kuboresha viwango vya huduma za afya na kuimarisha afya na ustawi wa watu barani Afrika.
Programu hiyo ya mafunzo inajumuisha washiriki 16 kutoka nchi 15 za Afrika, zikiwemo Ghana, Zimbabwe, Burkina Faso na Namibia.
Mafunzo hayo yanahusisha kozi mbalimbali, zikiwemo maelekezo ya kinadharia juu ya misingi na viwango vya dawa ya nyuklia na tiba ya mionzi. Pia ni pamoja na mafunzo ya kuigizia na ya vitendo katika kupanga matibabu, na kudhibiti na kuhakikisha ubora wa matibabu.
Vilevile, mafunzo hayo yanahusisha utafiti wa mifano halisi kuhusu saratani na uvimbe wa kawaida barani Afrika, pamoja na mihadhara maalumu ya wataalamu mashuhuri wa China katika fizikia ya matibabu, dawa za nyuklia na tiba ya mionzi.
Wataalamu wa fizikia wa tiba ya mionzi hubeba jukumu muhimu katika kupima na kubainisha ugonjwa kwa mionzi na matibabu ya magonjwa kama saratani na uvimbe.
China, kwa ushirikiano na IAEA, imetoa uungaji mkono wa teknolojia ya dawa za nyuklia, msaada wa kitaalamu, na mafunzo kwa wataalam kutoka nchi kadhaa za Afrika, zikiwemo Ethiopia, Nigeria na Morocco.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma