Wanafunzi Wakenya waliomwandikia barua Rais Xi na kupokea majibu yake waeleza namna ya Reli ya SGR ya Mombasa-Nairobi inavyoleta mageuzi ya kiuchumi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 06, 2024

Baadhi ya wanafunzi wa Kenya wanaosoma Chuo Kikuu cha Jiaotong cha Beijing, China ambao hapo awali walimwandikia barua Rais Xi Jinping wa China na kupokea jibu lake wameeleza kuwa reli ya SGR ya Mombasa-Nairobi iliyojengwa na Shirika la Madaraja la China imeleta mageuzi makubwa katika sekta za uchumi na usafirishaji nchini Kenya.

Wanafunzi hao walimwandikia barua Rais Xi mwezi Oktoba mwaka jana baada ya kumaliza masomo yao katika chuo hicho, wakieleza shukrani zao kwake kwa kuja na Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja ambalo limeleta manufaa makubwa kwa watu na nchi mbalimbali duniani ikiwemo Kenya ambayo imenufaika na miradi ya ushirikiano wa pande mbili ikiwemo miundombinu hususan reli hiyo ya SGR ya Nairobi-Mombasa ambako wanafanya kazi na fursa za ufadhili wa masomo ambazo wao ni moja ya wanufaika.

Tarehe 17, Januari, Rais Xi aliwajibu barua yao hiyo, kwa namna ambayo mmoja wa wanafunzi hao Jamlick Mwangi aliielezea kama “barua ndefu sana na ya kibinafsi” ambapo Xi alisema kwamba amefurahi kuona Wakenya hao wameunganishwa na China kupitia "njia hiyo ya furaha", ambayo ni rejea ya reli hiyo ya SGR.

Wakizungumza kwenye mahojiano ya hivi karibuni na People’s Daily Online, wanafunzi hao Mwangi na mwenzake Washington Aburiri ambao kwa sasa wamerudi tena katika Chuo Kikuu cha Jiaotong kuongeza ujuzi baada ya hapo awali kuhitimu chuoni hapo, wamesema, reli hiyo imeleta mambo mengi mapya ikiwemo mambo ya kisasa, ufanisi na kasi hivyo kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji na uchumi kwa ujumla.

Aburiri amesema kuwa, kwa kulinganisha reli hiyo ya SGR na reli zilizokuwepo zamani nchini Kenya, reli ya SGR ni ya kisasa zaidi, kwa sababu kadhaa, moja; kasi yake, kwamba reli hiyo ina kasi zaidi kuliko iliyokuwepo awali, pili; huduma ni za kisasa zaidi, akieleza kuwa zinafanyika kiotomatiki ikilinganishwa na reli ya awali.

“Kwa ujumla ninaweza sema ni ya kisasa zaidi kuliko ilivyokuwa awali” amesema Aburiri ambaye kwa sasa anasoma Shahada ya Uzamili katika Lojistiki na Usimamizi wa Uhandisi katika chuo hicho.

Aburiri amesema, wananchi hususuan wachuuzi wamepata kuiamini reli hiyo, wamekuwa na imani kwenye huduma zinazotolewa, kasi na uhakika wake, na kwamba kadri wanavyozidi kupata imani ndivyo wanavyozidi kupendekezana miongoni mwao kuhusu reli hiyo hali ambayo imepelekea shehena ya mizigo kuongezeka muda hadi muda.

Kwenye barua ya majibu ya Rais Xi, aliirejelea reli hiyo kama “njia ya furaha” ambapo katika mahojiano Mwangi, anayesoma shahada ya uzamili katika uhandisi wa ujenzi amesema ni “njia ya furaha”, kwa kuleta usafiri bora na wenye ufanisi na kuchochea shughuli za kibiashara na uchumi kwa ujumla nchini Kenya.

“Ni barabara ya furaha… kwa kuridhika kwa watu wanaoitumia, hivyo inaleta furaha zaidi” amesema Mwangi huku akiongeza kuwa reli hiyo imetoa fursa za kazi ambapo wafanyakazi wengi ni wenyeji hasa katika maeneo ya uendeshaji na matengenezo.

Mwangi amesema kuwa, huduma za reli hiyo zimekuwa fanisi na za kasi zaidi, ambapo muda wa usafiri wa abiria kwenda na kurudi kati ya Mombasa hadi Nairobi umepunguzwa kutoka saa 6 hadi 4 huku ule wa uchukuzi wa mizigo ukiwa umepunguzwa kutoka saa 8 hadi 6.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha