China kuweka hatua za kulipiza dhidi ya kampuni za kijeshi za Marekani kwa kuliuzia silaha eneo la Taiwan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 19, 2024

BEIJING - China imeamua kuweka hatua za kulipiza dhidi ya kampuni tisa za kijeshi za Marekani kwa kuliuzia silaha eneo la Taiwan ambalo ni sehemu ya China, uamuzi uliotolewa kwenye tovuti ya wizara ya mambo ya nje ya China siku ya Jumatano umeeleza.

Uamuzi huo umesema kwamba hivi karibuni Marekani imetangaza tena mpango wa kuliuzia silaha eneo la Taiwan, kitendo ambacho kinakiuka vibaya kanuni ya kuwepo kwa China moja na taarifa tatu za pamoja za China na Marekani, kinaingilia mambo ya ndani ya China na kudhuru mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi ya China.

Kwa mujibu wa Vifungu vya 3, 4, 6, 9 na 15 vya Sheria ya China ya Vikwazo Dhidi ya Mambo ya Nje, China imeamua kuchukua hatua zifuatazo za kulipiza dhidi ya Shirika la Sierra Nevada, Stick Rudder Enterprises LLC, Shirika la Cubic, S3 AeroDefense, TCOM, Limited Partnership, TextOre, Kundi la Kampuni za Planate Management, ACT1Federal na Exovera:

Mali zao zinazohamishika, zisizohamishika na aina nyingine zote za mali nchini China zitazuiliwa.

Mashirika na watu binafsi nchini China watapigwa marufuku kujihusisha katika miamala, ushirikiano au shughuli zingine na kampuni tajwa hapo juu.

Uamuzi huo umeanza kufanya kazi kuanzia tarehe 18 Septemba 2024.

Katika kujibu swali kuhusu mipango hiyo ya hivi karibuni ya Marekani ya kuuza silaha kwa eneo hilo la Taiwan la China, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian ameuambia mkutano na waandishi wa habari kwamba uuzaji huo wa silaha wa Marekani kwa Taiwan unakiuka vibaya kanuni ya kuwepo kwa China moja na taarifa tatu za pamoja za China na Marekani, hasa Taarifa ya Agosti 17 Mwaka 1982; unashambulia vibaya mamlaka ya nchi na maslahi ya usalama ya China; unadhuru uhusiano wa China na Marekani pamoja na amani na utulivu katika Mlango-Bahari wa Taiwan; na kutoa ishara ya makosa kwa nguvu ya mafarakano ya kutaka "Taiwan Ijitenge".

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha