Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping atoa wito wa mafanikio, michango mikubwa zaidi ya China kwa amani na maendeleo ya binadamu
Rais Xi Jinping wa China, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC), akihutubia katika dhifa ya kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, mji mkuu wa China, Septemba 30, 2024. (Xinhua/Xie Huanchi)
BEIJING - Rais Xi Jinping jana Jumatatu wakati akihutubia dhifa iliyofanyika kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China (PRC), amesema watu wa China watapata mafanikio makubwa zaidi na kutoa michango mikubwa zaidi katika lengo tukufu la amani na maendeleo ya binadamu.
Siku ya Kitaifa ya China inaadhimishwa leo Oktoba Mosi.
Kwenye hotuba yake, Rais Xi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC), kwa niaba ya Kamati Kuu ya CPC na Baraza la Serikali la China, kwanza ametoa pongezi nyingi kwa watu wa makabila yote ya China, maafisa na askari wa Jeshi la Ukombozi wa Umma la China (PLA) na Jeshi la Polisi la China, na kwa vyama na watu wengine wa kisiasa wasiotokana na CPC.
Rais Xi ametoa salamu za dhati kwa wananchi wa mikoa ya utawala maalum ya Hong Kong na Macao, katika eneo la Taiwan, na Wachina wa ng'ambo. Pia ametoa shukrani za dhati kwa nchi marafiki na marafiki wa kimataifa wanaojali na kuunga mkono maendeleo ya Jamhuri ya Watu wa China.
Rais Xi amesisitiza umuhimu wa kutekeleza kikamilifu, kwa uaminifu na kwa uthabiti sera ya Nchi Moja, Mifumo Miwili, ambayo chini yake watu wa Hong Kong husimamia Hong Kong na watu wa Macao husimamia Macao, zote zikiwa na kiwango kikubwa cha kujiamulia mambo yao.
"Taiwan ni sehemu muhimu ya ardhi ya China," Rais Xi amesema, akitoa wito wa juhudi za kuzidisha mabadilishano na ushirikiano wa kiuchumi na kitamaduni katika Mlango-Bahari wa Taiwan na kupinga kwa uthabiti shughuli za kujitenga zinazolenga "Kujitenga kwa Taiwan."
Akibainisha kuwa watu wa nchi zote wanaishi kwenye Dunia moja na wana mustakabali mmoja, Rais Xi ametoa wito kwa juhudi za kuhimiza ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja wa binadamu.
Baada ya miaka 75 ya juhudi kubwa, ujenzi wa mambo ya kisasa wa China umefunua matarajio mazuri, amesema Rais Xi, huku akitoa tahadhari dhidi ya hatari na changamoto zinazowezekana katika safari iliyoko mbeleni.
"Lazima tuendelee kuwa makini na hatari zinazoweza kutokea na kujiandaa vyema," Rais Xi amesema, akihimiza juhudi za kushinda kwa uthabiti hali ya kutokuwa na uhakika na hatari na changamoto zisizotarajiwa.
Viongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na wa serikali ya China, Xi Jinping, Li Qiang, Zhao Leji, Wang Huning, Cai Qi, Ding Xuexiang, Li Xi na Han Zheng wakihudhuria dhifa ya kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, mji mkuu wa China, Septemba 30, 2024. (Xinhua/Huang Jingwen)
Waziri Mkuu wa China Li Qiang, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akiongoza dhifa ya kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, mji mkuu wa China, Septemba 30, 2024. (Xinhua/Li Xueren)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma