Kiwanda cha Tesla cha Shanghai, China chafikia uzalishaji wenye mafanikio ya kihistoria wa magari milioni 3

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 12, 2024

Gari la milioni 3 lililozalishwa na Kiwanda kikubwa cha Magari cha Tesla cha Shanghai likitoka kwenye mstari wa kuunganisha sehemu za magari mjini Shanghai, mashariki mwa China, Oktoba 11, 2024. (Xinhua)

Gari la milioni 3 lililozalishwa na Kiwanda kikubwa cha Magari cha Tesla cha Shanghai likitoka kwenye mstari wa kuunganisha sehemu za magari mjini Shanghai, mashariki mwa China, Oktoba 11, 2024. (Xinhua)

SHANGHAI - Gari la milioni 3 lililozalishwa na Kiwanda kikubwa cha Shanghai cha Kampuni ya Tesla limetoka kwenye mstari wa kuunganisha sehemu za gari kiwandani jana siku ya Ijumaa, kikifikia hatua mpya katika dhamira ya kampuni hiyo ya Marekani kuendelea sambamba na sekta ya magari yanayotumia nishati mpya ya China.

Gari hilo, aina ya Y linalotumia umeme kikamilifu, limetoka kwenye mstari wa kuunganisha sehemu za gari kiwandani saa 12 jioni, kampuni hiyo imesema.

Kiwanda hicho cha Tesla cha Shanghai, ambacho ni kiwanda cha kwanza cha giga cha kuzalisha magari nje ya Marekani, kilianza kujengwa Januari 2019, na kuzalisha gari lake la kwanza mwezi Desemba mwaka huo.

Kiwanda hicho kilizalisha magari yake ya kwanza milioni 1 katika kipindi cha zaidi ya miezi 30, huku ikichukua miezi takriban 13 kwa uzalishaji wake kupanda kutoka milioni 2 hadi milioni 3, kampuni hiyo imeeleza.

Robo tatu za kwanza za mwaka huu zimeshuhudia kiwanda hicho kikizalisha magari 675,000, yakichukua zaidi ya nusu ya magari yote yaliyozalisjwa na kampuni hiyo katika kipindi hicho kote duniani, Tesla imesema.

Theluthi moja ya magari hayo milioni 3 yaliyozalishwa na kiwanda hicho yameuzwa kwa masoko nje ya China Bara, yakiwemo ya nchi za Ulaya na Asia-Pasifiki, kampuni hiyo imesema.

Mwezi Mei mwaka huu, kampuni hiyo ya Marekani iliweka jiwe la msingi kwenye kiwanda chake cha mega mjini Shanghai kuzalisha betri zake za kuhifadhi nishati za Megapacks. Kiwanda hicho kipya kinatarajiwa kuanza kufanya kazi katika robo ya kwanza ya mwaka ujao.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha