Lugha Nyingine
Viongozi wa Med9 wahimiza usimamishaji wa mapigano na juhudi za kidiplomasia katika Mashariki ya Kati
Viongozi wa Mkutano wa Kilele wa Med9 wakihudhuria mkutano na waandishi wa habari mjini Paphos, Cyprus, Oktoba 11, 2024. (Picha na George Christophorou/Xinhua)
NICOSIA - Viongozi wa nchi tisa za Mediterania za Umoja wa Ulaya (EU) zinazojulikana kwa jina la Med9, baada ya Mkutano wa Kilele wa 11 wa Med9 jana Ijumaa, uliofanyika katika Mji wa Paphos, Magharibi mwa Cyprus, wametoa wito wa kusimamisha mara moja mapigano katika Mashariki ya Kati na kuhimiza kuanzishwa tena juhudi za kidiplomasia ili kushughulikia migogoro inayoendelea katika eneo hilo.
Viongozi hao wamesema katika taarifa yao kwamba "hali inayoendelea katika Mashariki ya Kati inatia wasiwasi sana, wakitaka "kusimamisha mara moja mapigano" na kutoa misaada ya kibinadamu kwa Lebanon haraka iwezekanavyo.
"Tunatoa wito kwa wahusika wote kujizuia na kushiriki katika juhudi za upatanishi ili kutuliza mivutano," viongozi hao wa Med9 wamesema katika taarifa yao hiyo baada ya mkutano huo wa mchana kutwa.
Kundi hilo pia limethibitisha kuunga mkono maazimio yote ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mashariki ya Kati na kuahidi kufanya kazi pamoja ili kushawishi sera pana za Umoja wa Ulaya kuhusu masuala ya eneo hilo.
Huku kukiwa na mgogoro unaozidi kuongezeka katika Mashariki ya Kati, vita kati ya Russia na Ukraine, na shinikizo la kisiasa, kiuchumi na kijamii linaloendelea, muundo huu wa mfumokazi wa kikanda ni muhimu katika kujenga mwitikio wa Ulaya kwa changamoto za pamoja, taarifa hiyo imesema.
Cyprus ambayo kwa sasa ni nchi mwenyekiti wa zamu wa kundi hilo la Med9, ndiyo ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo uliohudhuriwa na wakuu wa nchi au serikali kutoka Ufaransa, Ugiriki, Italia, Croatia, Malta, Slovenia na Hispania, huku Ureno ikiwakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje. Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen pia amehudhuria.
Mbali na viongozi wa Umoja wa Ulaya, Mfalme Abdullah II wa Jordan ameshiriki katika mkutano sambamba wa kujadili masuala ya kikanda. Mchango wa Jordan katika kushughulikia mgogoro wa Mashariki ya Kati umetambuliwa kuwa muhimu.
Viongozi wa Mkutano wa Kilele wa Med9 wakiwa katika picha ya pamoja mjini Paphos, Cyprus, Oktoba 11, 2024. (Picha na George Christophorou/Xinhua)
Mfalme Abdullah II (Kulia) wa Jordan akizungumza na Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen kwenye Mkutano wa Kilele wa Med9 mjini Paphos, Cyprus, Oktoba 11, 2024. (Picha na George Christophorou/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma