Lugha Nyingine
Biashara ya nje ya Mkoa wa Guangdong, China yafikia rekodi ya juu
Watu wakitazama gari linalotumia nishati mpya kwenye Maonyesho ya Canton mjini Guangzhou, Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, Oktoba 15, 2024. (Xinhua/Lu Hanxin)
GUANGZHOU - Mkoa wa Guangdong, ambao ni mkoa wenye nguvu kubwa ya kiuchumi wa China, umeripoti rekodi mpya katika biashara yake ya nje kwa robo tatu za kwanza za mwaka huu, huku uagizaji na uuzaji wake nje bidhaa ukifikia yuan trilioni 6.75 (dola za Kimarekani kama bilioni 951), kiasi ambacho kimeongezeka kwa asilimia 11.1 kuliko mwaka jana wakati kama huo.
Mauzo ya nje ya mkoa huo yalifikia yuan trilioni 4.39 katika kipindi hicho, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.1 mwaka hadi mwaka, huku uagizaji nje bidhaa ukifikia yuan trilioni 2.36, ikiwa ni ukuaji wa mwaka hadi mwaka wa asilimia 15, Zhang Ke, naibu mkurugenzi wa idara ya Guangdong ya Mamlaka ya Forodha ya China, amesema katika mkutano na waandishi wa habari jana Jumatatu.
Biashara ya nje ya mkoa huo wa Guangdong sasa inawakilisha asilimia 20.9 ya jumla ya biashara yote ya nje ya China, ukidumisha nafasi yake ya uongozi na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa China. Kiwango cha ukuaji wa biashara ya nje ya mkoa huo kilipita wastani wa kote nchini kwa asilimia 5.8.
“Rekodi hii mpya ya kihistoria ya kiwango cha biashara ya nje ya Guangdong kwa kipindi hicho imedhihirisha uthabiti na ustawi mkubwa wa kiuchumi wa mkoa,” Zhang amesema.
Mji wa Shenzhen, kitovu cha China cha teknolojia katika mkoa huo wa Guangdong, pia umepata rekodi ya juu kwa kuwa na thamani ya jumla ya biashara ya nje ya yuan trilioni 3.37 katika kipindi kama hicho, ikiongezeka kwa asilimia 20.9 mwaka hadi mwaka, idara ya forodha ya Shenzhen imesema.
Uagizaji na uuzaji nje bidhaa wa Shenzhen kwa pamoja ulifikia rekodi ya juu, huku mauzo ya nje yakiongezeka kwa asilimia 19.7 mwaka hadi mwaka na kufikia yuan trilioni 2.14 na uagizaji nje biadhaa wenye thamani ya Yuan trilioni 1.23, ikiongezeka kwa asilimia 23.1 mwaka hadi mwaka.
Kampuni za kibinafsi katika mji huo wa Shenzhen ndizo zilizotoa mchango katika ukuaji huo, kwa asilimia 70.9 ya jumla ya biashara ya nje ya mji huo katika robo tatu hizo za kwanza. Zimerekodi thamani ya jumla ya uuzaji na uagizaji nje bidhaa ya Yuan trilioni 2.39, ikiwa ni ongezeko la asilimia 30.8 mwaka hadi mwaka.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma