

Lugha Nyingine
China yawasilisha msaada muhimu wa matibabu kwa Lebanon huku kukiwa na mgogoro unaopamba moto
Wafanyakazi wakipakua shehena ya msaada wa dharura wa matibabu kutoka China kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Rafik Hariri huko Beirut, Lebanon, Oktoba 21, 2024. (Xinhua/Bilal Jawich)
BEIRUT - China imewasilisha shehena ya msaada wa dharura wa matibabu kwa Lebanon siku ya Jumatatu, wakati nchi hiyo ya Mashariki ya Kati ikikabiliana na vifo na majeruhi kutokana na migogoro inayoendelea ya kuvuka mpaka na Israel, ambapo shehena hiyo, yenye masanduku 3,601 ya mashine za ganzi, mirija ya kupumulia na gauni za kuvaa wakati wa operesheni, imewasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Rafik Hariri wa Beirut.
Kwenye uwanja huo wa ndege, Balozi wa China nchini humo Qian Minjian na Waziri wa Afya wa Lebanon Firass Abiad walishiriki kwenye hafla ya kukabidhi shehena hiyo ya msaada ambapo Balozi Qian amesisitiza kuwa mgogoro huo umeleta mateso makubwa kwa watu wa Lebanon, na kusababisha idadi kubwa ya vifo, majeruhi na wakimbizi.
"China inaiunga mkono kithabiti Lebanon katika kudumisha mamlaka ya nchi, usalama na heshima ya kitaifa, na inapinga vikali mashambulizi yoyote ya kiholela dhidi ya raia," balozi huyo wa China amesema, akielezea matumaini yake kwamba msaada huo wa dharura wa matibabu utasaidia kutoa unafuu kwa mfumo wa huduma ya afya wa Lebanon ulio katika shinikizo.
Kwa upande wake Abiad akizungumza kwa niaba ya serikali ya Lebanon, ametoa shukrani kwa msaada huo wa ubinadamu uliotolewa kwa wakati na China.
Amepongeza uungaji mkono wa China kwa Lebanon kila wakati, haswa ametaja msaada uliotolewa na China wakati wa vita vya Lebanon dhidi ya janga la UVIKO-19 na katika madhara ya mlipuko wa bandari ya Beirut Mwaka 2020.
Michango ya China inawakilisha ishara muhimu ya mshikamano na Lebanon, ameongeza.
Tangu Septemba 23, Jeshi la Israel limeanzisha mashambulizi makali ya upigaji mabomu kutoka angani dhidi ya Lebanon, ikiashiria kuongezeka kwa hatari kwa mgogoro dhidi ya Hezbollah.
Wizara ya Afya ya Lebanon ilisema, tangu Oktoba 2023, migogoro kati ya Hezbollah na vikosi vya Jeshi la Israel imesababisha vifo vya watu zaidi ya 2,400 na wengine zaidi ya 11,000 kujeruhiwa.
Balozi wa China Qian Minjian (kulia) na Waziri wa Afya wa Lebanon Firass Abiad wakishiriki kwenye hafla ya kukabidhi shehena ya msaada wa dharura wa matibabu kutoka China kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Rafik Hariri huko Beirut, Lebanon, Oktoba 21, 2024. (Xinhua/Bilal Jawich)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma