Lugha Nyingine
IMF yadumisha makadirio ya ukuaji wa uchumi duniani Mwaka 2024 katika asilimia 3.2, yakionya juu ya mivutano ya siasa za kijiografia
Mchumi Mkuu wa IMF Pierre-Olivier Gourinchas akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Washington, D.C., Marekani, Oktoba 22, 2024. (Xinhua/Hu Yousong)
WASHINGTON - Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limedumisha makadirio yake ya ukuaji wa uchumi duniani Mwaka 2024 kwa asilimia 3.2, ikiendana na makadirio yake ya awali ya Julai, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Mtazamo wa Uchumi wa Dunia (WEO) iliyotolewa jana Jumanne, ikibainisha kuwa kiwango cha kutokuwa na uhakika kinachozunguka mtazamo huo wa uchumi wa dunia kiko juu.
"Serikali mpya zitakazochaguliwa (karibu nusu ya watu wote duniani wameshapiga au watapiga kura mwaka 2024) zinaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sera ya mambo ya biashara na fedha," imesema ripoti hiyo.
"Zaidi ya hayo, kurejea kwa hali tete ya soko la fedha wakati wa majira ya joto kumezua hofu ya zamani kuhusu udhaifu uliofichika. Hii imeongeza wasiwasi juu ya msimamo unaofaa wa sera ya fedha -- hasa katika nchi ambako mfumuko wa bei unaendelea na dalili za kupungua zinajitokeza," imesema zaidi.
Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa kuongezeka zaidi kwa tofauti za siasa za kijiografia kunaweza kuleta madhara katika biashara, uwekezaji na mtiririko huru wa mawazo. "Hii inaweza kuathiri ukuaji wa muda mrefu, kutishia uhimilivu wa minyororo ya usambazaji, na kuleta changamoto kwa benki kuu," imesema.
Katika kujibu swali kutoka Shirika la Habari la China, Xinhua, Mchumi Mkuu wa IMF Pierre-Olivier Gourinchas amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba kuongezeka kwa mivutano ya siasa za kijiografia ni "jambo ambalo tunajali sana," akibainisha kuwa kuna athari katika pande mbili.
"Moja ni, kwa hakika, kama utaongeza ushuru, kwa mfano, kati ya maeneo tofauti, hiyo itavuruga biashara, ambayo itatenga rasilimali vibaya, ambayo itapunguza shughuli za kiuchumi," amesema Gourinchas. "Lakini pia kuna pande husika ambazo zinatokana na hali ya kutokuwa na uhakika inayoongezeka kuhusiana na sera ya biashara ya baadaye, na pia itashinikiza uwekezaji, kuzuia shughuli za kiuchumi na matumizi," ameendelea.
Mchumi huyo mkuu amebainisha kuwa IMF imepata athari katika viwango vya pato duniani ya takriban asilimia 0.5 Mwaka 2026. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukuaji wa uchumi duniani unakadiriwa kushika kasi, lakini kuna matarajio yanayodhoofika na vitisho vinavyoongezeka.
Mtazamo wa ukuaji ni thabiti sana katika nchi zenye masoko yanayoibukia na nchi zinazoendelea, karibu asilimia 4.2 mwaka huu na ujao, huku kukiwa na ufanisi mzuri unaoendelea kutoka Asia inayoibukia, imesema ripoti hiyo.
Mchumi Mkuu wa IMF Pierre-Olivier Gourinchas (wa pili, kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Washington, D.C., Marekani, Oktoba 22, 2024. (Xinhua/Hu Yousong)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma