

Lugha Nyingine
Viongozi wa BRICS wapitisha taarifa ya pamoja kufuatia mkutano wa kilele mjini Kazan, Russia
KAZAN, Russia - Viongozi wa nchi za BRICS wametoa taarifa ya pamoja inayohusu masuala mbalimbali kuanzia mageuzi ya Umoja wa Mataifa (UN) hadi migogoro inayoendelea duniani, kufuatia mkutano wa viongozi wa kundi hilo uliofanyika Jumatano mjini Kazan ambapo taarifa hiyo inajumuisha vipengele 134 kwa jumla.
"Tunasisitiza tena kuunga mkono mageuzi ya Umoja wa Mataifa katika pande zote, ikiwa ni pamoja na Baraza lake la Usalama, kwa nia ya kuufanya kuwa wa kidemokrasia, wakilishi, wenye mchango na fanisi," taarifa hiyo inasema. Hii inahusisha kupanua uwakilishi wa nchi zinazoendelea ili kukabiliana vyema na changamoto za kimataifa, imeongeza.
Aidha, viongozi hao wamesisitiza kulaani kwao kabisa ugaidi wa aina zote na kutaka kupitishwa mara moja kwa Mkataba Jumuishi juu ya Ugaidi wa Kimataifa ndani ya Umoja wa Mataifa.
Sambamba na mageuzi hayo muhimu, nchi wanachama wa BRICS zimetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuchukua jukumu muhimu katika usimamizi wa kimataifa wa Akili Bandia.
Taarifa hiyo pia limejikita katika migogoro duniani ikiwa ni pamoja na ile ya Mashariki ya Kati na Ukraine.
"Tunaendelea kuwa na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ghasia na kuendelea kwa migogoro katika sehemu tofauti za dunia," taarifa hiyo inasoma. Viongozi wa nchi za BRICS wamesisitiza dhamira yao ya kusuluhisha migogoro kwa amani kupitia njia za diplomasia.
Viongozi wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu mvutano unaoendelea katika Ukanda wa Gaza na kutaka kusimamishwa mara moja kwa mapigano na kusitishwa kwa uhasama wote.
Viongozi hao wamebainisha umuhimu wa kuanzishwa kwa nchi ya Palestina ndani ya mipaka inayotambulika kimataifa ya Juni 1967, na wameelezea kuunga mkono uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa.
Nchi hizo wanachama pia zimekumbushia misimamo yao juu ya mgogoro wa Ukraine, na "zimebainisha kwa shukrani mapendekezo muhimu" yenye lengo la suluhu ya amani ya mgogoro huo kwa njia za diplomasia.
Viongozi hao wa BRICS pia wameeleza wasiwasi wao mkubwa juu ya athari mbaya za vikwazo haramu vya upande mmoja kwa uchumi wa dunia, wakisema kuwa vinaathiri vibaya ukuaji wa uchumi, nishati, usalama wa chakula na kuzidisha umaskini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma