Tanzania na kampuni kutoka China zasaini makubaliano ya ujenzi wa daraja la mita 390

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 24, 2024

DAR ES SALAAM - Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Ujenzi wa Mawasiliano ya China (CCCC) zimetia saini makubaliano ya kujenga daraja lenye urefu wa mita 390 kwenye eneo la Jangwani katika mji wa bandari wa nchi hiyo wa Dar es Salaam, mamlaka za serikali ya Tanzania zimesema katika taarifa.

Taarifa iliyotolewa Jumatano na Wizara ya Ujenzi ya Tanzania ilisema kuwa, Wakala wa Barabara wa Tanzania amesaini makubaliano hayo kwa niaba ya serikali na kampuni hiyo kutoka China siku ya Jumanne, ambapo Waziri wa Wizara hiyo ya Ujenzi Innocent Bashungwa alihudhuria na kushuhudia hafla ya kusaini.

Ujenzi wa daraja hilo utakaogharimu dola milioni 36 za Marekani utafanyika sambamba na ujenzi wa matuta ya kulinda kingo za Mto Msimbazi, kutokana na eneo la daraja hilo kukumbwa na mafuriko wakati wa majira ya mvua. Mradi huo utasimamiwa na Ofisi ya Rais inayohusika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Baada ya kukamilika, Daraja la Jangwani litawapa ahueni madereva zaidi ya 500,000 wanaotumia daraja hilo kila siku.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha