Viongozi wa BRICS wadhamiria kujenga utaratibu wa dunia wa kidemokrasia na wenye pande nyingi: Putin

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 25, 2024

Rais wa Russia Putin

Rais wa Russia Putin akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari katika siku ya mwisho ya Mkutano wa 16 wa Viongozi wa Nchi za BRICS mjini Kazan, Russia Oktoba 24. (Xinhua/Cao Yang)

MOSCOW - Nchi za BRICS zina dhamira ya kujenga utaratibu wa dunia wa kidemokrasia na wenye pande nyingi, Rais wa Russia Vladimir Putin amesema siku ya Alhamisi, kwenye mkutano na waandishi wa habari katika siku ya mwisho ya Mkutano wa 16 wa Viongozi wa Nchi za BRICS mjini Kazan, Russia.

Rais Putin amesema kuwa Azimio la Kazan, lililoidhinishwa katika mkutano huo, linaelezea ajenda chanya kwa siku za baadaye, habari kutoka ikulu ya Kremlin imesema.

"Ni muhimu kwamba azimio hilo lithibitishe dhamira ya mataifa yetu yote kujenga utaratibu wa dunia ulio wa kidemokrasia, jumuishi na wa pande nyingi zenye usawa kwa kuzingatia sheria za kimataifa na Katiba ya Umoja wa Mataifa," ameeleza.

Rais Putin ameongeza kuwa nchi za BRICS ziko wazi kwa wote wanaofaidika maadili yake, na zinadhamiria kutafuta suluhu za pamoja bila shinikizo la nje au mbinu finyu.

Kundi hilo halifanyi kazi kwa njia iliyofungwa, amesisitiza katika mkutano huo na waandishi wa habari.

Rais huyo wa Russia amethibitisha kuwa viongozi wa BRICS wamekubaliana juu ya orodha ya nchi washirika wa BRICS.

"Baadhi ya nchi ambazo zimeshiriki katika shughuli hizi zimewasilisha mapendekezo na maombi yao ya ushiriki kamili katika kundi la BRICS," Putin ameongeza.

Amesema kuwa nchi za BRICS hazijaunda na haziundi njia mbadala wa mfumo wa malipo ya kimataifa, SWIFT, akiongeza kuwa suala hilo bado ni muhimu, na nchi wanachama wanasonga mbele kuelekea kwenye matumizi ya sarafu zao zenyewe.

Amesema nchi wanachama wa BRICS kwa sasa wanatumia Mfumo wa Utumaji Ujumbe wa Mambo ya Fedha ulioundwa na Benki Kuu ya Russia.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha