

Lugha Nyingine
Mradi wa kuzalisha umeme kwa jotoardhi unaofadhiliwa na China kuongeza upatikanaji wa nishati safi nchini Kenya
Rais wa Kenya William Ruto (Mbele) akiendesha tingatinga wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya jotoardhi katika Kaunti ya Nakuru, Kenya, Oktoba 24, 2024. (Xinhua/Han Xu)
NAIROBI - Azma ya Kenya ya kupatikana nishati ya kijani kwa wote imepata hamasa siku ya Alhamisi kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa megawati 35 (MW) kwa nishati ya jotoardhi katika Kaunti ya Nakuru, iliyoko umbali wa kilomita takriban 200 kaskazini-magharibi mwa Nairobi, mji mkuu wa Kenya.
Ukipangwa kutekelezwa ndani ya miezi 17 kwa dola za Kimarekani takriban milioni 90, mradi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme wa Megawati 35 kwa nishati ya Jotoardhi cha Orpower 22 utaharakisha kubadili muundo wa nishati kuwa wa kijani, kuimarisha uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na kuhimiza ukuaji wa uchumi wa Kenya, maafisa waandamizi wa Kenya wamesema.
Rais wa Kenya William Ruto aliongoza hafla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, ambao utatekelezwa na Kundi la Kampuni za Kaishan, kampuni ya kimataifa yenye makao yake makuu mjini Shanghai, China, kupitia muundo wa ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.
Rais Ruto amesema ujenzi wa kituo hicho cha kuzalisha umeme kwa nishati ya jotoardhi unaashiria dhamira ya Kenya kufikia lengo la kihistoria la gridi ya taifa ya umeme ambayo ni ya kijani kwa asilimia 100 ifikapo Mwaka 2030 na unaonesha dhamira yake ya kufungua uwezo mkubwa wa jotoardhi nchini Kenya ili kuendeleza ukuaji wa uchumi.
Amesema kuwa Kenya imeweka mazingira wezeshi kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika vyanzo vya nishati mbadala kama vile jua, upepo na jotoardhi, hali ambayo inalingana na ajenda yake ya ukuaji wa viwanda wa kijani.
Kwa sasa, Kenya imetumia Megawati 950 pekee kati ya Megawati 10,000 za nishati ya jotoardhini zilizopo nchini, Rais Ruto amesema, akisisitiza kuwa wawekezaji kama Kundi la Kampuni za Kaishan watakuwa muhimu katika maendeleo endelevu ya chanzo hicho safi cha nishati.
Yan Tang, meneja mkuu wa Kundi la Kampuni za Kaishan, amesema kuwa kupitia ushirikiano na serikali ya Kenya na jumuiya za wenyeji, kampuni hiyo inatarajia kutekeleza miradi ya nishati ya jotoardhi na hidrojeni ya kijani, ili kuhimiza viwanda vya Kenya kutimiza lengo la kutotoa kaboni.
Rais wa Kenya William Ruto akizungumza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia jotoardhi katika Kaunti ya Nakuru, Kenya, Oktoba 24, 2024. (Xinhua/Han Xu)
Rais wa Kenya William Ruto akizungumza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia jotoardhi katika Kaunti ya Nakuru, Kenya, Oktoba 24, 2024. (Xinhua/Han Xu)
Rais wa Kenya William Ruto akifungua pazia kuonesha bango la maandishi ya jiwe la msingi kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia jotoardhi katika Kaunti ya Nakuru, Kenya, Oktoba 24, 2024. (Xinhua/Han Xu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma