

Lugha Nyingine
Rwanda yazindua kampeni ya upandaji miti kwa wingi
Maelfu ya Wanyarwanda wameshiriki katika kampeni kubwa ya upandaji miti siku ya Jumamosi katika Kijiji cha Kamamana, Wilaya ya Rwamagana, mashariki mwa Rwanda, na kuendeleza lengo la taifa hilo la kupanda miti milioni 65 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa fedha.
Ikiongozwa na Wizara ya Mazingira ya Rwanda, kampeni hiyo inalenga kuongeza misitu, kusaidia uhifadhi wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kulinda rasilimali za maji na kuimarisha maisha ya wenyeji.
Katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo ambapo miti 25,000 ilipandwa kwenye ardhi ya ukubwa wa hekta 17, Waziri wa Mazingira wa Rwanda, Valentine Uwamariya amewahamasisha wakazi kuendeleza utamaduni wa kupanda miti na kutunza miti iliyopandwa ili kuhakikisha ukuaji wake na matokeo yanayokusudiwa. Pia amesisitiza jukumu la pamoja la kulinda misitu ya Rwanda.
Takwimu kutoka wizara hiyo zinaonesha kuwa misitu sasa inachukua asilimia 30.4 ya eneo lote la ardhi la Rwanda, ikiwa ni jumla ya hekta 724,695.
Ili kulinda misitu zaidi, serikali imewataka wananchi kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa kutumia vyanzo mbadala vya nishati kama vile biogesi, gesi na umeme.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma