Rais wa Msumbiji atoa wito wa kuungwa mkono kimataifa kufuatia nchi yake kuwa na changamoto baada ya uchaguzi

(CRI Online) Oktoba 29, 2024

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi Jumatatu ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuiunga mkono nchi hiyo kwa ajili ya kuleta utulivu na amani kufuatia uchaguzi wa hivi karibuni.

Nyusi ametoa wito huo wakati alipokutana na mabalozi wa kigeni mjini Maputo, akisisitiza jukumu muhimu la utulivu wa kisiasa katika maendeleo ya Msumbiji na umuhimu wa kulinda amani baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2024.

Nyusi amelaani vikali ghasia za hivi karibuni kwenye maandamano ya kupinga uchaguzi nchini humo, akisema zimesababisha uharibifu na makabiliano ya moja kwa moja na vyombo vya usalama. Pia amekumbusha muktadha wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 9, akisema malalamiko yanashughulikiwa na Baraza la Katiba, chombo chenye jukumu la kuthibitisha matokeo ya uchaguzi huo.

Amesisitiza kuwa juhudi za kudumisha utulivu wa ndani zinapaswa kukamilishwa na uungwaji mkono wa kimataifa hasa kutokana na changamoto tata za kiuchumi na kijamii za nchi hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha