

Lugha Nyingine
Mchuano ni mkali kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Marekani wiki moja kabla ya uchaguzi
Picha hii iliyopigwa Septemba 10, 2024 ikionyesha Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris (Kulia) na Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump wakiwa kwenye mdahalo wa wagombea urais mjini Philadelphia, Marekani. (Xinhua/Li Rui)
WASHINGTON – Tovuti ya habari za uchaguzi ya Marekani, Real Clear Politics inaonesha kuwa kuna mchuano mkali kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais wa Marekani, wiki moja kabla ya wamarekani kupiga kura kumchagua rais ajaye. Mgombea wa chama cha Republican Donald Trump anamzidi mgombea wa Chama cha Democratic Kamala Harris kwa wastani wa asilimia 0.4 katika kura za maoni hadi kufikia Jumanne.
Trump anaongoza kwa alama chache sana katika majimbo mengi yenye ushindani mkali (swing states), yakiwemo Georgia, Arizona, Pennsylvania, Wisconsin na North Carolina, huku Harris akiongoza kwa nusu pointi katika Jimbo la Michigan.
Majimbo hayo huenda yakaamua matokeo ya uchaguzi, na wagombea wote wawili wamekuwa wakifanya kampeni kikamilifu, wakihudhuria mikutano ya hadhara kuwasilisha hoja zao kwa wapiga kura.
"Kinyang'anyiro cha urais bado ni kikali, lakini Harris amekuwa akimzidi matumizi Trump kwa tofauti ya 2 au 3 hadi 1 katika matangazo ya kampeni," Msomi Mwandamizi wa Taasisi ya Brookings, Darrell West ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Mfumuko wa bei na uchumi ni miongoni mwa masuala makuu. Wakati Rais Joe Biden na Makamu wa Rais Harris wameweza kusimamia uchumi wenye kiwango cha chini cha ukosefu wa ajira, wapiga kura wengi wamekasirishwa na mfumuko wa bei ambao umedumu wakati wa utawala wa sasa.
Mbali na hilo, timu ya kampeni ya Trump imekuwa ikishutumu utawala wa Biden-Harris kwa kusababisha ongezeko kubwa la uhalifu katika maeneo ya mijini.
Bado haijulikani wapiga kura ambao bado hawajaamua watampigia kura nani, watafanya nini.
"Wapiga kura wengi ambao hawajaamua nani watampigia kura hawatapiga kura kabisa," Clay Ramsay, mtafiti katika Idara ya mambo ya Kimataifa na Usalama katika Chuo Kikuu cha Maryland, ameliambia Xinhua, akiongeza kuwa watu ambao huenda hawatapiga kura, kulingana na chaguzi zilizopita, wanachukua asilimia kubwa ya watu wazima.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma