Watoto zaidi ya milioni 2.8 wa Sudan wakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu huku mgogoro wa kivita ukiendelea

(CRI Online) Oktoba 31, 2024

Mashirika ya kimataifa na mamlaka za Sudan zimesema watoto zaidi ya milioni 2.8 walio chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu huku migogoro ya kivita ikiendelea kuiteketeza nchi hiyo.

Shirika la kimataifa lisilo la kiserikali la Save the Children limesema kwenye ripoti jana Jumatano kuwa watoto hao, ambao sasa wamekimbia makazi yao kote nchini Sudan, "watakosa mambo muhimu ya utotoni, ikiwemo chanjo, maji safi, huduma ya afya, chakula cha lishe bora, na kujisitiri dhidi ya joto na baridi kali."

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya nusu ya watu milioni 11 waliokimbia makazi yao, au milioni 5.8, ni watoto walio na umri wa chini ya miaka 18, huku wengi wao wakiishi katika kambi za wakimbizi, makazi yasiyo rasmi, shule zenye msongamano, au majengo mengine ya umma.

Wakati huo huo, mashirika maarufu ya kibinadamu katika jimbo la katikati mwa nchi hiyo la Gezira, ambalo linashuhudia mashambulizi yanayoongezeka, yameonya kuwa watoto ndiyo waathirika wakuu wa wimbi la sasa la ghasia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha