

Lugha Nyingine
Wafanyabiashara na wajasiriamali kutoka Tanzania waeleza furaha, shukrani kwa nchi yao kuwa mgeni wa heshima wa maonyesho ya CIIE
Banda la Tanzania likionekana kwenye Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 6, 2024. (People’s Daily Online)
Wafanyabiashara na wajasiriamali kutoka Tanzania wanaoshiriki Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) mjini Shanghai, Mashariki mwa China wameeleza furaha kubwa kwa nchi yao kuwa mgeni wa heshima wa maonyesho hayo na namna walivyojipanga kutumia vema fursa hiyo kunadi chapa ya 'made in Tanzania'.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Banda la Tanzania la maonyesho hayo katika Ukumbi wa Taifa wa Mikutano na Maonyesho wa China (Shanghai), washiriki hao pia wametoa shukrani kwa waandaaji wa maonyesho hayo na Serikali ya China kwa kuipa Tanzania hadhi hiyo maalum na pia kuwezesha bidhaa za Tanzania kuingia kwa urahisi na kwa unafuu wa kodi kwenye soko kubwa la China.
Akizungumza kwenye banda la Tanzania Jackson Joel, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Akros, kampuni inayojishughulisha na biashara ya ubanguaji na uuzaji wa korosho, amesema fursa hiyo ya Tanzania kuwa nchi mgeni wa heshima ni ya kipekee, yenye thamani na maalum na kwamba kampuni yake imejipanga kuitumia kikamilifu kupata wateja na makubaliano mengi ya kibiashara na wateja watarajiwa wa China.
“Ni fursa ya kipekee, ni heshima kubwa na ukitazama kati ya nchi nyingi waalikwa sisi Tanzania tumepewa heshima hiyo. Ni jambo kubwa sana” amesema Joel.
Amesema, tayari kwa siku mbili tu za kuwepo kwenye maonyesho hayo ameshapata miadi mitatu yenye uwezekano wa kupata wabia wa kununua bidhaa na watembeleaji wengi wanachukua mawasiliano yake na kuweka oda za uwezekano wa kununua bidhaa au kufanya biashara na kampuni yake.
Joel pia ameeleza kufurahia fursa ya bidhaa za Afrika kuingia soko la China chini ya unafuu wa ushuru uliotangazwa na Serikali ya China chini ya Mkutano wa Kilele wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Septemba mwaka huu.
Naye mjasiriamali Elis Thomas wa Kampuni ya EPC, kampuni inayouza nje bidhaa mbalimbali, amesema ni mara yake ya kwanza kushiriki maonyesho hayo kwani huko nyuma alijaribu bila mafanikio kutokana na changamoto za kitaratibu. Lakini mwaka huu ameona Serikali ya China imerahisisha sana ushiriki wao na kila kitu kimeenda kwa urahisi na utaratibu hadi kufika kwenye maonyesho.
“Ubalozi wa China nchini Tanzania umeturahisishia sana. Kuanzia upatikanaji wa visa hadi uingiaji wa bidhaa zetu China. Kila kitu kimeenda vizuri” amesema Thomas.
Maonyesho hayo ya CIIE yakiwa na kaulimbiu ya “Zama Mpya, Mustakabali wa Pamoja” yamefunguliwa rasmi jana Jumanne Novemba 5 na yamepapangwa kuendelea hadi Novemba 10 yakishirikisha nchi, maeneo na mashirika ya kimataifa 132. Tanzania ni nchi mgeni wa heshima wa maonyesho hayo sambamba na nchi za Ufaransa, Malaysia, Nicaragua, Saudi Arabia na Uzbekistan.
Jackson Joel akionyesha bidhaa zake kwenye Banda la Tanzania la Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 6, 2024. (People’s Daily Online)
Watembeleaji wakiulizia bidhaa kwenye Banda la Tanzania la Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 6, 2024. (People’s Daily Online)
Watembeleaji wakiwa kwenye Banda la Tanzania la Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 6, 2024. (People’s Daily Online)
Watembeleaji wakiulizia bidhaa kwenye Banda la Tanzania la Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 6, 2024. (People’s Daily Online)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma