Afisa wa Burundi aeleza furaha kwa nchi yake kushiriki kwa mara ya kwanza katika CIIE, ikihamasishwa na msamaha wa ushuru wa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 07, 2024

Bulimaso Alfred (kushoto), konsuli wa kwanza wa ubalozi wa Burundi mjini Beijing na Kamariza Estella (kulia), mwonyeshaji bidhaa, wakionyesha mafuta ya kupakaa ya moringa, yaliyotengenezwa kutokana na mmea wa kienyeji uitwao moringa kwenye banda la Burundi la Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) mjini Shanghai, Novemba, 6, 2024. (People's Daily Online)

Bulimaso Alfred (kushoto), konsuli wa kwanza wa ubalozi wa Burundi mjini Beijing na Kamariza Estella, mwonyeshaji bidhaa, wakionyesha mafuta ya kupakaa ya moringa, yaliyotengenezwa kutokana na mmea wa kienyeji uitwao moringa kwenye banda la Burundi la Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) mjini Shanghai, Novemba, 6, 2024. (People's Daily Online)

Maonyesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) ni jukwaa muhimu sana kwa dunia nzima kwani ni fursa nzuri kwa kampuni na bidhaa zao kutambulika, kujulikana na kuonekana kwa dunia nzima, Bulimaso Alfred, konsuli wa kwanza wa ubalozi wa Burundi mjini Beijing, China amesema, akielezea furaha kwa nchi yake kushiriki kwa mara ya kwanza katika maonyesho hayo ya saba ya mwaka huu, ikihamasishwa na msamaha wa ushuru wa China kwa nchi zenye uchumi mdogo zikiwemo za Afrika.

Akizungumza na People’s Daily Online kwenye banda la Burundi la maonyesho hayo, Bulimayo amesema Burundi lazima iwepo kwenye maonyesho hayo kwa kuwa watu wengi hawajasikia bidhaa kutoka kwa nchi yake kwa sababu walichokuwa wakipata kutoka kwenye habari ni mambo ya zamani kuhusu matatizo ya kisiasa, lakini sasa ni zama mpya, Burundi inamaanisha biashara.

“Lazima tuwe hapa, hili ni soko muhimu sana kwa dunia nzima na kwa Burundi pia, hivyo hatuwezi kubaki nyuma, lazima tuje hapa, tupate maonyesho haya, tulete kampuni zetu zitambulike kwa dunia nzima, lazima zionekane” Bulimaso amesema.

Ameongeza kuwa, Burundi na China zimetia saini mkataba wa makubaliano kuhusu kilimo, ili bidhaa za kilimo kutoka Burundi ziweze kuingia katika soko kubwa la China bila kulipa ushuru.

“Kwa hiyo ni muhimu sana sisi kuwa hapa, ili kuonyesha watu bidhaa zetu” amesema Bulimaso, akiongeza kuwa nchi yake imeleta bidhaa kama vile kahawa, mafuta ya kupakaa ya moringa, mafuta yaliyokamuliwa kutoka kwenye mbegu za mmea wa kienyeji uitwao moringa, mafuta ya parachichi na chai.

Bulimaso pia amepongeza ahadi ya China kuondoa ushuru wa forodha kwenye bidhaa bora za kilimo zinazoagizwa kutoka Afrika wakati wa mkutano wa kilele mwaka huu wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), akisema kuwa itawezesha kampuni na bidhaa nyingi za Afrika kulifikia soko kubwa la China huku zikipata ukuaji mkubwa wa kasi.

“Tangu zamani tulikuwa na mtiririko wa mwelekeo mmoja wa bidhaa, bidhaa kutoka China kwenda Burundi na nchi nyingine nyingi za Afrika, lakini sasa itabidi tulete bidhaa nyingi kutoka Burundi na Afrika hadi China” amesema huku akipongeza hatua hiyo kuwa ni muhimu na yenye kuleta urahisi na uwezeshaji wa biashara kati ya pande hizo mbili.

Picha hii ikionyesha banda la Burundi la Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE), mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 6, 2024. (People's Daily Online)

Picha hii ikionyesha banda la Burundi la Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE), mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 6, 2024. (People's Daily Online)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha