

Lugha Nyingine
Kampuni za uchimbaji madini za China nchini Zambia zaanzisha shirikisho ili kuongeza mchango wa sekta hiyo
LUSAKA – Kampuni za China za sekta ya madini nchini Zambia zimeanzisha rasmi Shirikisho la Kampuni za Uchimbaji Madini za China nchini Zambia (CMEAZ) siku ya Jumanne yenye lengo la kuimarisha mchango wa kampuni hizo kwenye sekta ya madini katika nchi hiyo.
Shirikisho hilo limezinduliwa rasmi kwenye hafla iliyohudhuriwa na Balozi wa China nchini Zambia Han Jing, maafisa waandamizi wa serikali ya Zambia pamoja na wawakilishi kutoka kampuni za China za uchimbaji madini nchini humo.
Katika hotuba yake, balozi wa China amezipongeza kampuni hizo kwa kuunda shirikisho hilo na mchango wao katika uhusiano kati ya China na Zambia, akisema kuanzishwa kwa shirikisho hilo ni hatua kubwa katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya madini ambao ulianza Mwaka 1998 wakati kampuni za China zilipowekeza kwenye mgodi wa shaba wa Chambishi.
"Baada ya miaka ya zaidi 20 ya maendeleo, ushirikiano wa uchimbaji madini kati ya China na Zambia umeshuhudia ongezeko la hatua kwa hatua katika idadi ya kampuni zinazoshiriki, kiwango kinachopanuka na ngazi inayoongezeka kila mara," amesema.
Kwa mujibu wake, sasa kuna kampuni zaidi ya 20 za uchimbaji madini zinazowekezwa kwa mtaji kutoka China nchini Zambia zikiwa na uwekezaji wa jumla ya dola za kimarekani wa zaidi bilioni 3.5.
Takwimu kutoka kwa shirikisho hilo zinaonyesha kuwa, kampuni wanachama wa shirikisho hilo zililipa kodi dola za Kimarekani zaidi ya milioni 260 Mwaka 2023 na kwa sasa zinaajiri watu wenyeji zaidi ya 15,000.
Balozi Han amesema wafanyakazi wenyeji wapatao 1,000 hupata mafunzo ya ufundi wa kazi kila mwaka katika kituo cha mafunzo ya wafanyakazi cha CMEAZ.
Waziri wa Maendeleo ya Migodi na Madini wa Zambia Paul Kabuswe amesema kuanzishwa kwa shirikisho hilo ni hatua nyingine muhimu katika kuongeza ushirikiano wa uchimbaji madini katika kuendeleza utafiti wa madini na upatikanaji wa haki za kuchimba madini.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Tobias Musonda, mkurugenzi wa mipango na habari katika wizara hiyo, waziri huyo wa Zambia amesema hiyo itasaidia Zambia kutimiza lengo la kufikia uzalishaji wa shaba za uzito wa tani milioni tatu ifikapo mwaka 2031.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma