Waziri Mkuu wa Ethiopia azindua kituo cha uchunguzi na utafiti wa jinai kilichoungwa mkono na China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 18, 2024

ADDIS ABABA - Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amezindua Kituo cha Uchunguzi na Utafiti wa Jinai cha Jeshi la Polisi la Ethiopia siku ya Jumamosi mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Akiongea kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo hicho, Abiy amesema kituo hicho kitasaidia askari polisi wa nchi hiyo kufanya uchunguzi wa kisayansi wa kidijitali na upimaji wa DNA pamoja na kufanya uchambuzi wa uhalifu tata.

“Mwaka mmoja na nusu tu uliopita, wakati kipimo cha DNA kilipohitajika, tulilazimika kutegemea rasilimali za nje,” Waziri Mkuu huyo amebainisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii baada ya kuzindua kituo hicho.

Abiy amesema kituo hicho ni matokeo ya dhamira ya serikali yake kufanya vyombo vya utekelezaji sheria kuwa vya kisasa na kuvipa teknolojia na maarifa muhimu. Pia amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanaakisi mageuzi makubwa ambayo nchi hiyo imefanya katika sekta ya ulinzi na usalama katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

"Leo hii, Ethiopia imeanzisha taasisi yenye uwezo wa kushughulikia changamoto zinazohusiana na DNA ndani ya nchi huku pia ikihudumia nchi jirani," amesema waziri mkuu huyo, akikumbushia kuwa nchi hiyo imekuwa ikituma sampuli nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi wa DNA hadi hivi karibuni.

Hafla hiyo ya uzinduzi ilishirikiwa na maafisa waandamizi wa serikali, maafisa wa jeshi la polisi na wanadiplomasia kutoka nchi mbali mbali.

Ubalozi wa China nchini Ethiopia katika salamu zake za pongezi umesema kituo hicho kitakidhi siyo tu mahitaji ya Ethiopia bali pia ya nchi za Afrika Mashariki na Afrika nzima.

Kwa mujibu wa Ubalozi huo, China imetoa uungaji mkono wa kiufundi na vifaa kwa ujenzi wa kituo hicho kipya cha uchunguzi na utafiti wa jinai.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha