

Lugha Nyingine
Afrika kutumia vizuri fursa ya kujiunga na G20
(Xinhua/Wang Tiancong)
Kabla ya mkutano wa kilele wa G20 wa mwaka huu, wataalamu walisema kuwa, nchi za Afrika zinapaswa kutumia vizuri fursa ya kujiunga na kundi la nchi 20 (G20) ili kuhimiza biashara na uwekezaji na nchi zenye nguvu zaidi duniani.
Sizo Nkala, mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Afrika na China ya Chuo Kikuu cha Johannesburg alipohojiwa na China Daily alisema kuwa, Umoja wa Afrika kujiunga na G20 ni hatua muhimu ya kuifanya Afrika iongeze zaidi kutambuliwa kwake kwenye jukwaa la kimataifa, na kutoa fursa kwa Afrika kujadiliana kwa usawa na nchi tajiri.
Mkutano wa kilele wa G20 wa mwaka huu uliofanyika Rio de Janeiro, Brazil umeshirikisha kwa mara ya kwanza Umoja wa Afrika ukiwa mwanachama wake. Mwaka uliopita kundi hilo lilipokea Umoja wa Afrika kuwa mwanachama wake wa kudumu.
“Kujiunga na G20 kwa Umoja wa Afrika kutaleta ushawishi kwa hali ya uchumi wa dunia. Afrika itakaa pamoja na nchi tajiri na kuelezea ufuatiliaji wake na maslahi yake, na kutoa sauti kwa ajili yake yenyewe,” alisema Nkala.
Alan Mukoki, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Biashara na Viwanda la Afrika Kusini alisema, anakaribisha Umoja wa Afrika kupata nafasi ya mwanachama wa kudumu katika G20, lakini Afrika itatumia kwa namna gani fursa hii nzuri bado inatakiwa kufuatiliwa.
Amesema, ni lazima Afrika kutumia nafasi hii mpya kuhimiza biashara kati yake na nchi zenye nguvu zaidi, na kutafuta uwekezaji wa kuendeleza Bara la Afrika.
Mikatekiso Kubayi, mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Mazungumzo ya Dunia ya jumuiya ya washauri bingwa ya Afrika Kusini, anakubali maoni ya Mukoki.
Alisema, “Waafrika wakitaka kupata tena nafasi muhimu katika mambo ya ushirikiano wa pande nyingi, wanapaswa kufanya vizuri mambo yao wenyewe. Afrika inatakiwa kufanya mazungumzo na nchi kubwa ili kunufaisha bara hilo. Dunia imeelewa kuwa Bara la Afrika halipuuziki kwani thamani ya jumla ya uzalishaji wake imefikia dola za kimarekani trilioni 3.1, na idadi ya watu wake imekuwa zaidi ya bilioni 1.4.
Kubayi alisema, nchi za Afrika na nchi nyingi za Dunia ya Kusini zinahitaji teknolojia na mitaji ili kuzisaidia kupita mpito kwa usawa hadi kutumia nishati safi na kuacha hatua kwa hatua nishati ya visukuku, na kundi la G20 linaweza kuzisaidia kwa upande huo. Alisema, kundi la G20 pia linaweza kuisaidia Afrika kujiandaa kwa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Afrika Kusini itakuwa nchi mwenyekiti wa zamu wa G20 kuanzia Desemba 1, na kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa G20 mwakani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma