

Lugha Nyingine
UN yatafuta fedha zaidi kwa ajili ya mpango wa mwitikio wa kibinadamu wa Sudan mwaka 2025
Umoja wa Mataifa (UN) unashirikiana na Sudan kuongeza ufadhili wa kifedha kwa ajili ya mpango wa mwitikio wa kibinadamu wa mwaka 2025, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Habari la Sudan (SUNA) ikimnukuu ofisa mwandamizi wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher.
Kwenye mkutano wake na mkuu wa Kamisheni ya Misaada ya Kibinadamu ya Sudan, Mona Nourel Daim katika Jimbo la Port Sudan, Fletcher amesisitiza haja ya juhudi za pamoja kukabili janga la Sudan linalozidi kuongezeka.
“Tutafanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja na serikali ya Sudan kuchangia katika ongezeko la ufadhili wa kifedha kwa ajili ya mpango wa mwitikio wa kibinadamu wa mwaka 2025” Fletcher amenukuliwa na SUNA akisema.
Kwa upande wake, Bi. Nourel Daim amesisitiza kiwango cha janga hilo, akionya kuwa michango ya wafadhili mwaka 2024 haikukidhi mahitaji. “Ufadhili wa kifedha kutoka kwa wafadhili wakati wa Mwaka 2024 uko chini ya matarajio, licha ya ukweli kwamba Sudan inapitia hali mbaya zaidi ya kibinadamu” amesema.
Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuongeza uungaji mkono kwa ajili ya mpango huo wa mwitikio wa mwaka 2025 ili kutekeleza miradi muhimu na kupunguza mateso miongoni mwa watu waliokimbia makazi yao.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma