Rais wa Zimbabwe atoa wito wa uungaji mkono wa kimataifa katika kutatua masuala ya madeni

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 26, 2024

HARARE - Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa siku ya Jumatatu katika hotuba yake kuu kwenye kongamano la saba la jukwaa la mazungumzo la ngazi ya juu mjini Harare, mji mkuu wa Zimbabwe ametoa wito kwa wakopeshaji na washirika wa maendeleo kuisaidia nchi hiyo kushughulikia deni lake la nje, ambalo linadhoofisha maendeleo yake ya kiuchumi.

Mnangagwa amesema Zimbabwe imepata maendeleo makubwa katika kutekeleza mageuzi ya uchumi, ya sekta ya umma, na ya utawala ili kufungua njia kwa ajili ya kutatua deni la dola bilioni 21 za Kimarekani la nchi hiyo linalojumuisha deni la nje la dola bilioni 13 na deni la ndani la dola bilioni 8.

Amesema kutekelezwa kwa mafanikio kwa mkakati wa kumaliza marupurupu na utatuzi wa deni ni muhimu kwa Zimbabwe kupata ufadhili mpya wa nje wenye masharti nafuu ambao ni muhimu kwa ajili ya kufikia maendeleo ya kiuchumi.

"Tangu kuanzishwa kwa mchakato wa muundo wa jukwaa la mazungumzo mwaka 2022, tumepata maendeleo makubwa, huku kukiwa na kuongezeka kwa maelewano, uaminifu na imani katika mpango huu," Mnangagwa amesema.

"Ninatoa wito kwa taasisi za fedha za kimataifa, washirika wa maendeleo, wadai wetu, na jumuiya ya kimataifa kuendelea kuunga mkono mchakato wa kumaliza marupurupu na utatuzi wa deni." amesema

Mchakato wa kumaliza marupurupu na utatuzi wa deni unasimamiwa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Akinwumi Adesina wakati Rais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano akiwa ni mwezeshaji wa ngazi ya juu.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Adesina amesema ujumbe wa wafanyakazi wa IMF unatarajiwa kuandaa mfumo wa SMP wakati wa ujumbe wake wa kawaida wa wafanyakazi nchini Zimbabwe mwezi Januari mwaka ujao.

Amesikitika kwamba vikwazo vya miaka mingi vya nchi za Magharibi kwa Zimbabwe vimezidisha deni la nchi hiyo na kutaka kufanya juhudi za pamoja kutatua msukosuko huo wa deni kwa haraka.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha