Rais Biden asema makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah "yameundwa kuwa" ya kudumu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 27, 2024

Rais wa Marekani Joe Biden akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani White House mjini Washington, D.C., Marekani, Novemba 26, 2024. (Xinhua/Hu Yousong)

Rais wa Marekani Joe Biden akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani White House mjini Washington, D.C., Marekani, Novemba 26, 2024. (Xinhua/Hu Yousong)

WASHINGTON - Rais wa Marekani Joe Biden amesema Jumanne kwamba makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa siku 60 kati ya Israel na Hezbollah nchini Lebanon yaliyopendekezwa na Marekani, ambayo "yameundwa kuwa" ya kudumu, yameanza kutekelezwa rasmi saa 10:00 alfajiri leo Jumatano kwa saa za huko (2:00 asubuhi GMT).

"Chini ya makubaliano yaliyofikiwa leo (jana Jumanne), kuanzia saa 10 alfajiri kesho (leo Jumatano) kwa saa za huko, mapigano katika mpaka wa Lebanon na Israel yatamalizika," Biden amesema katika hotuba yake aliyoitoa akiwa Rose Garden, Ikulu ya Marekani White House.

"Haya yameundwa kuwa usimamishaji wa kudumu wa uhasama. Kile kilichobaki kwa Hezbollah na makundi mengine ya kigaidi hakitaruhusiwa," ameongeza.

"Katika muda wa siku 60 zijazo, Israel itaondoa hatua kwa hatua vikosi vyake vilivyobaki, na raia wa pande zote mbili hivi karibuni wataweza kurejea salama katika jumuiya zao na kuanza kujenga upya makazi yao," Biden amesema.

Ameongeza kuwa, Israel "inabaki na haki ya kujilinda" katika tukio ambalo "Hezbollah au upande mwingine wowote" utavunja makubaliano hayo mapya yaliyotangazwa, ambayo yameidhinishwa na baraza la mawaziri la Israeli siku hiyo hiyo.

Kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa na Marekani na Ufaransa ya kutangaza makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano, nchi hizo mbili zimesema "taarifa hiyo itaweka mazingira ya kurejesha utulivu wa kudumu na kuruhusu wakaazi katika nchi zote mbili kurejea salama kwenye makazi yao ya pande zote za Mstari wa Bluu."

Mstari huo wa Bluu ni alama ya mpaka wa mstari uliochorwa na Umoja wa Mataifa tarehe 7 Juni, Mwaka 2000 ambao ulilenga kutenganisha majeshi ya Israel na Lebanon.

Biden katika hotuba yake amesema makubaliano hayo "yanaunga mkono mamlaka ya Lebanon, na hivyo yanaashiria mwanzo mpya wa Lebanon." Amesema hakuna wanajeshi wa Marekani watakaotumwa kusini mwa Lebanon.

Biden amesema makubaliano hayo kati ya Israel na Hezbollah "yanatuleta karibu zaidi katika kutambua ajenda thabiti" ambayo amekuwa akiitafuta kwa eneo la Mashariki ya Kati katika kipindi chote cha uongozi wake, ambayo inatimiza matarajio halali ya watu wa Palestina ya kuanzisha taifa lao wenyewe, kuilinda Israel dhidi ya tisho la ugaidi na kufikia lengo la kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Saudi Arabia na Israel.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha