

Lugha Nyingine
Umoja wa Mataifa wataka kusimamisha mapigano mara moja, na kuanzisha mazungumzo nchini Syria
Watu wakisubiri nje ya hospitali baada ya makundi yenye silaha kufyatua makombora kwenye jengo la bweni katika mji wa Aleppo, kaskazini mwa Syria, Novemba 29, 2024. (Str/Xinhua)
DAMASCUS - Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu nchini Syria Adam Abdelmoula ametaka kusitisha vitendo vya uhasama mara moja mjini Aleppo kaskazini magharibi mwa Syria na kuanzisha mazungumzo kati ya pande husika.
Kuongezeka kwa ghasia hivi karibuni mjini Aleppo kuanzia Jumatano "kumesababisha vifo vya raia wasio na hatia, wakiwemo wanawake na watoto, uharibifu wa miundombinu ya kiraia, na kusimamishwa kwa huduma muhimu," Abdelmoula amesema katika taarifa yake.
Hii imekuja "wakati ambapo watu wasiohesabika, wengi wao ambao tayari wamevumilia huzuni ya kulazimika kukimbia makazi yao, sasa wanalazimika kukimbia kwa mara nyingine, wakiacha nyuma nyumba zao na shughuli zao," Abdelmoula ameongeza.
"Tunatoa wito kwa pande zote za mgogoro kusitisha mara moja uhasama na kutoa kipaumble katika kulinda raia na wafanyakazi wa kutoa msaada," amesema, akiongeza, "Watu wa Syria hawapaswi kustahimili mateso zaidi, na tunatoa wito wa kufanya mazungumzo."
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza dhamira ya jumuiya ya kibinadamu katika kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa watu walioathirika.
Siku ya Jumatano, mashambulizi makubwa ya waasi yalitikisa maeneo ya pembezoni mwa mji huo wa Aleppo, yakiwa ni mashambulizi ya kwanza muhimu tangu mwaka 2016. Mashambulizi hayo yametekelezwa na muungano wa makundi ya waasi, hasa Hayat Tahrir al-Sham, shirika la mrengo wa itikadi kali linalohusishwa na al-Qaida kwa lengo la kupenya maeneo yanayoshikiliwa na serikali. Mashambulizi hayo yamepiga hatua huku yakiwezesha kushikiliwa kwa maeneo muhimu ya Aleppo na Idlib.
Likikabiliwa na idadi kubwa ya wapiganaji na mashambulizi mengi, Jeshi la Syria lilitangaza kupeleka tena kwa muda vikosi vyake. Vyombo vya habari vya serikali ya Syria na Shirika la Kufuatilia Haki za Binadamu la Syria, shirika la kufuatilia vita lenye makao yake makuu nchini Uingereza, vimeripoti Jumapili kwamba vikosi vya serikali vilianzisha mashambulizi katika eneo la kaskazini la Hama, na kukomboa maeneo muhimu kutoka kwa makundi hayo ya waasi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma