

Lugha Nyingine
Mkutano wa Kuifahamu China Mwaka 2024 wasisitiza mageuzi, kunufaika na maendeleo
![]() |
Li Shulei, Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mkuu wa Idara ya Uenezi ya Kamati Kuu ya CPC, akisoma barua ya pongezi ya Rais Xi Jinping wa China kwa mkutano wa Kuifahamu China Mwaka 2024 na kutoa hotuba kuu katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo mjini Guangzhou, Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, Desemba 3, 2024. (Xinhua/Zhang Ling) |
GUANGZHOU - Mkutano wa Kuifahamu China Mwaka 2024, unaojikita katika ujenzi wa mambo ya kisasa wa China na fursa mpya kwa dunia, umefunguliwa siku ya Jumanne mjini Guangzhou, mji mkuu wa Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China.
Mkutano huo wa mwaka huu, wenye kaulimbiu ya "Kuendelea Mageuzi Hadi Mwisho – Ujenzi wa Mambo ya Kisasa wa China na Fursa Mpya kwa Maendeleo ya Dunia," unakutanisha pamoja washiriki zaidi ya 600 wakiwemo wanasiasa, maafisa, wasomi, wajumbe wa kigeni na wawakilishi wa vyombo vya habari.
Li Shulei, Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mkuu wa Idara ya Uenezi ya Kamati Kuu ya CPC, alisoma barua ya pongezi ya Rais Xi Jinping wa China kwenye mkutano huo na kutoa hotuba kuu katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.
Mkutano huo, uliopangwa kuendelea hadi leo Jumatano, unajumuisha semina sita zinazofanyika sambamba, mabaraza 14 ya mada mahsusi, mijadala miwili ya wanajopo ya ndani, na maonyesho ya mafanikio ya juhudi za ujenzi wa mambo ya kisasa wa China.
Mkutano huo pia utaangazia uhai na uwezo wa kiuchumi wa Eneo la Ghuba Kuu ya Guangdong-Hong Kong-Macao kama kichocheo kikuu cha ujenzi wa mambo ya kisasa wa China na kutazama fursa za maendeleo kwenye sekta mbalimbali katika zama ya akili mnemba za kidijitali, uchumi wa anga ya chini, na nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora.
Mada zingine ni pamoja na kulinda na kurithi urithi wa kihistoria na kitamaduni katika ujenzi wa mambo ya kisasa, vilevile ushirikiano wa Kusini na Kusini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma