

Lugha Nyingine
Afrika Kusini yazindua uenyekiti wa zamu wa G20 ikiwa na dhamira katika ujumuishaji, uendelevu wa dunia
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa uenyekiti wa zamu wa G20 wa Afrika Kusini mjini Cape Town, Afrika Kusini, Desemba 3, 2024. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)
CAPE TOWN - Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amezindua rasmi uenyekiti wa zamu wa nchi hiyo wa Kundi la nchi 20 (G20) siku ya Jumanne, akitangaza dhamira ya nchi hiyo ya kuhimiza dunia iliyo jumuishi, yenye usawa, na endelevu zaidi.
Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa uenyekiti huo wa G20 mjini Cape Town, mji mkuu wa kibunge wa nchi hiyo, Ramaphosa ameeleza kuwa kuchukua huko kwa Afrika Kusini uenyekiti wa zamu kuanzia Desemba 1 ni hatua ya kihistoria kwa nchi ya kwanza ya Afrika kuongoza kundi hilo lenye ushawishi la nchi zenye uchumi mkubwa duniani.
"Uenyekiti wa G20 wa Afrika Kusini unakuja wakati ambapo dunia inakabiliwa na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na janga la mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usawa na umaskini, matarajio yanayopunguzwa ya ongezeko la uchumi duniani, na kukosekana kwa utulivu wa siasa za kijiografia," amesema. "Kwa kushirikiana na nchi wanachama wa G20 na kujenga ushirikiano katika jamii nzima, Afrika Kusini itatafuta kutumia kikamilifu nia na uwezo wa kimataifa kukabiliana na changamoto hizi."
Hasa, Afrika Kusini itaongoza kundi hilo kutafuta ukuaji jumuishi wa uchumi, kufikia haki ya kimataifa, kutokomeza umaskini na njaa, na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya mustakabali endelevu, amesema, akiongeza kuwa kwa kuakisi azma hiyo, Afrika Kusini imepitisha kaulimbiu ya "Mshikamano, Usawa na Uendelevu," kwa uenyekiti wake huo.
"Kulingana na kaulimbiu yetu, tutajaribu kuimarisha na kuendeleza juhudi za kimataifa za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo Mwaka 2030," Ramaphosa amesema. "Tutatumia wakati huu kuleta vipaumbele vya maendeleo vya Bara la Afrika na Nchi za Kusini kwa uthabiti zaidi kwenye ajenda ya G20."
Maeneo muhimu yatakayozingatiwa kwa uenyekiti wa Afrika Kusini ni pamoja na kuimarisha uwezo wa kupambana na majanga, kuhakikisha uhimilivu wa madeni kwa nchi zenye mapato ya chini, kuhamasisha ufadhili kwa ajili ya kubadilisha miundo ya nishati kwa haki, na kutumia kikamilifu madini muhimu kwa maendeleo jumuishi, amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma