

Lugha Nyingine
TAZARA yatangaza kusimamisha huduma ya treni ya abiria kwa siku 13 nchini Tanzania
Mamlaka ya Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA) imetangaza kusimamisha huduma ya treni ya abiria kwa siku 13 kuanzia tarehe 29 Novemba nchini Tanzania kutokana na kufungwa kwa njia nyingi za reli.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo, huduma hiyo imepangwa kurejeshwa tarehe 12 Desemba.
Afisa Uhusiano wa TAZARA Regina Tarimo, ameeleza sababu ya kusimamishwa kwa huduma hiyo kuwa ni kutokea kwa matukio kadhaa ambayo yamevuruga uwezo wa reli hiyo wa kutoa huduma salama.
Taarifa imesema katika kipindi cha mwezi uliopita, TAZARA imekabiliana na changamoto kumi za uendeshaji ikiwemo kuharibika kwa reli na treni za mizigo kuacha njia, hali ambayo imelazimu sehemu za reli kufungwa kwa ajili ya ukarabati.
Mamlaka hiyo imewahakikishia abiria kuwa sasa timu za ukarabati, wahandisi na wadau wanafanya bidii ili kurejesha huduma hizo za treni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma