Rais mteule wa Namibia aahidi umoja, maendeleo, uwajibikaji katika hotuba yake baada ya uchaguzi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 06, 2024

Rais Mteule wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Windhoek, Namibia, Desemba 5, 2024. (Picha na Musa C Kaseke/Xinhua)

Rais Mteule wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Windhoek, Namibia, Desemba 5, 2024. (Picha na Musa C Kaseke/Xinhua)

WINDHOEK - Rais mteule wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah amezungumza na vyombo vya habari siku ya Alhamisi kwenye mkutano na waandishi wa habari wa Chama cha South West Africa People's Organization (SWAPO), kufuatia ushindi wake wa kihistoria kwenye uchaguzi ambapo amesisitiza umuhimu wa uchaguzi, akisema kuwa kujitokeza kwa idadi kubwa ya wapiga kura na ushiriki wa amani na nidhamu wa Wanamibia ni ushahidi wa ukomavu wa demokrasia ya nchi hiyo.

"Tumemaliza tu punde uchaguzi wa kihistoria ulioonyesha hali ya uvumilivu wa kisiasa, uhimilivu, na dhamira imara kwa demokrasia," amesema.

Nandi-Ndaitwah ametambua mchango wa Wanamibia, hasa vijana, ambao wameipa chama cha SWAPO mamlaka ya kutawala, akisisitiza wajibu wa chama hicho katika kuheshimu uaminifu huo uliowekwa kwao.

Rais huyo mteule ametoa kwa umma maono yake ya utawala, akisisitiza ujumuishaji, uadilifu, na uwajibikaji. “Tunapojiandaa na kazi ya kutawala Namibia kwa miaka mitano ijayo, sina budi kuwakumbusha wote katika uongozi wa SWAPO kuanzia kwenye sehemu, matawi, wilaya na mikoa hadi ngazi ya taifa, kufanya kazi kwa bidii ili kurudisha upendo wa watu wetu kwa SWAPO," amesema.

Kwa mujibu wake, nguvu za SWAPO ziko kwa watu wa Namibia, na imani yao haipaswi kuharibiwa. "Kama mnavyofahamu, watu wengi wenye haki ya upiga kura ni vijana au wenye umri mdogo," amesema. "Vijana wa Namibia wametoa mchango mkubwa zaidi katika kukipa chama cha SWAPO mamlaka ya kutawala nchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, na tuna deni kwao."

Wakati huo huo, Nandi-Ndaitwah amewapongeza wale waliochaguliwa katika Bunge la Taifa. "Chama cha SWAPO ni chama ambacho kimeleta uhuru wa kisiasa kwa watu wa Namibia na lazima kuhakikisha kuwa uhuru wa kiuchumi unapatikana katika maisha yetu," amesema.

SWAPO, chama tawala cha Namibia, kimeshinda katika chaguzi zote mbili za rais na wabunge wa bunge la taifa zilizomalizika hivi karibuni. Chama hicho kimekuwa chama tawala cha Namibia tangu nchi hiyo ilipopata uhuru Mwaka 1990.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha