

Lugha Nyingine
Vyombo vya habari vya Russia vyasema Bashar al-Assad amewasili Moscow
Habari kutoka Shirika la Habari la Russia, TASS imesema aliyekuwa rais wa Syria, Bashar al-Assad na familia yake wamewasili Moscow nchini Russia, ambapo nchi hiyo imewapa hifadhi.
Kundi la upinzani la Syria limetangaza jana Jumapili, Desemba 8 kuwa limeingia Damascus, mji mkuu wa nchi hiyo na kupitia televisheni likasema kuwa limeikomboa Damascus na kupindua serikali ya al-Assad.
Wizara ya mambo ya nje ya Russia imetoa taarifa siku hiyo ikisema baada ya kufanya mazungumzo na pande zote za mapigano nchini Syria na kuagiza kukabidhi madaraka kwa amani, Bashar al-Assad ameamua kujiuzulu wadhifa wa urais wa Syria na kuondoka nchini humo.
Likinukuu taarifa kutoka Ikulu ya Russia, Klemrin, Shirika la TASS limesema kuwa Russia imewapa Bashar al-Assad na familia yake hifadhi kutokana na sababu ya kibinadamu.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Russia inaunga mkono siku zote kutafuta suluhu ya kisiasa kwa mgogoro wa Syria, na madhumuni ya Russia ni kurejesha mazungumzo chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma