Lugha Nyingine
Panda watatu waliozaliwa Ubelgiji warudi China
Picha hii iliyopigwa Desemba 10, 2024 ikionyesha keki zenye umbo la panda katika bustani ya wanyama ya Pairi Daiza mjini Brugelette, Ubelgiji. (Xinhua/Meng Dingbo)
BRUSSELS - Tian Bao, Bao Di, na Bao Mei, panda watatu waliozaliwa katika bustani ya wanyama ya Pairi Daiza nchini Ubelgiji, wamefunga safari ya kurejea China jana siku ya Jumanne, ikionyesha hatua muhimu katika mpango wa uhifadhi wa panda kati ya nchi hizo mbili.
Tian Bao, aliyezaliwa mwaka 2016, pamoja na wadogo wake, mapacha Bao Di na Bao Mei, waliozaliwa mwaka 2019, watajiunga na Kituo cha Uhifadhi na Utafiti wa Panda cha China mjini Bifengxia, Mkoani Sichuan. Huko, watashiriki katika miradi ya uhifadhi na uzalianaji.
Watu wakiwaaga panda katika bustani ya wanyama ya Pairi Daiza mjini Brugelette, Ubelgiji, Desemba 10, 2024. (Xinhua/Zhao Dingzhe)
Licha ya hali ya hewa ya baridi mwezi Desemba, watu karibu elfu moja walikusanyika kwenye bustani hiyo ya wanyama ili kuwaaga panda hao wapendwa. Wakiwa watulivu lakini wadadisi, panda hao watatu waliketi katika sanduku maalumu kwa ajili ya safari yao.
Kwenye hafla ya kuwaaga, Balozi wa China nchini Ubelgiji Fei Shengchao amesema: "Panda si tu ni wanyama wa kupendeza na adimu ambao wanaleta furaha kwa watu, lakini pia ni daraja linalounganisha hisia za watu na kuhimiza mawasiliano ya utamaduni. Ni alama ya dhamira ya pamoja ya China na Ubelgiji kulinda mazingira ya asili na kuishi nayo kwa mapatano."
Tangu walipowasili Ubelgiji mwaka 2014, wazazi wa panda hao watatu, Hao Hao na Xing Hui, wamekuwa wakivutia mamilioni ya watembeleaji huku wakitoa uelewa kuhusu ulinzi wa panda hao.
Watu wakiwaaga panda katika bustani ya wanyama ya Pairi Daiza mjini Brugelette, Ubelgiji, Desemba 10, 2024. (Xinhua/Zhao Dingzhe)
Eric Domb, mwanzilishi wa bustani hiyo ya wanyama ya Pairi Daiza, ameelezea fahari na huzuni kutokana na kuondoka kwa panda hao. "Tutaendelea kuwatunza panda kwa upendo wetu wote, kama tunavyofanya siku zote. Tutaendelea kujitahidi kuwasaidia kuzalisha vitoto vingi zaidi katika siku za usoni," amesema, akisisitiza dhamira ya bustani hiyo kwa uhifadhi wa panda.
Panda hao walianza kipindi chao cha karantini Novemba 11 ili kuhakikisha kuwa wanakuwa tayari kwa safari hiyo.
Gari lililowabeba panda Bao Di na Bao Mei likiondoka kwenye bustani ya wanyama ya Pairi Daiza mjini Brugelette, Ubelgiji, Des. 10, 2024. (Xinhua/Zhao Dingzhe)
Xing Hui na Hao Hao ambao ni wazazi wa panda hao vitoto watabakia bustani ya Pairi Daiza hadi mwaka 2029, wakiendelea na jukumu lao la kuwa mabalozi wa uhusiano kati ya China na Ubelgiji na kuhimiza mawasiliano ya kitamaduni na uelewa wa mazingira.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma