

Lugha Nyingine
Raia 65 wauawa kwenye shambulio la vikosi vya wanamgambo katika mji wa Omdurman, Sudan
Watu wakikagua nyumba iliyobomolewa katika shambulio la vikosi vya wanamgambo katika Mji wa Omdurman, Sudan, Desemba. 10, 2024. (Ofisi ya Habari ya Serikali ya Sudan ya Khartoum/kupitia Xinhua)
KHARTOUM – Serikali ya Sudan ilitangaza jana Jumanne huko Khartoum, kwamba Vikosi vya Uuungaji Mkono wa Haraka (RSF) vilipiga mizinga dhidi ya mji wa Omdurman, kaskazini mwa mji mkuu Khartoum na kusababisha Raia takriban 65 kuuawa.
"Wanamgambo wagaidi wakipiga mizinga dhidi ya raia wa eneo la Karani, wamefanya mauaji makubwa zaidi ya binadamu ya kuwaua watu zaidi ya 65 na mamia ya wengine wamejeruhiwa ambao wamejaa hospitalini," ofisi ya habari ya Serikali ya Sudan mjini Khartoum imesema katika taarifa.
Ahmed Osman Hamza, gavana wa Jimbo la Khartoum, alitembelea eneo lililoshambuliwa, ikiwa ni pamoja na kituo cha mabasi cha eneo la Karari kaskazini mwa Omdurman, ambapo basi la abiria lilipigwa na mizinga na kusababisha vifo vya watu 22, taarifa hiyo imeeleza.
Waathiriwa wengine wamekumbwa na shambulio la wakati mmoja ambalo lililenga soko karibu na kituo hicho cha basi na kituo cha afya, taarifa hiyo imesema.
Gavana huyo ameilaani RSF kwa kulenga raia wasio na silaha, akisema "shambulio hili linalenga kuwatia hofu raia ili waondoke kutoka maeneo salama," taarifa hiyo imemnukuu.
Ametoa wito kwa jumuiya na mashirika ya kimataifa kutekeleza jukumu lao katika kulinda raia ambao wanalengwa moja kwa moja na "wanamgambo" ndani ya nyumba zao, masoko na majengo ya matibabu.
Fath Al-Rahman Mohamed Al-Amin, mkuu wa Idara ya afya ya Serikali ya Sudani mjini Khartoum, amesema "hospitali za Omdurman zinaendelea kupokea watu ambao wamefariki au kujeruhiwa, huku wafanyakazi wa afya wakifanya juhudi kubwa kuokoa maisha ya majeruhi na kutoa huduma ya afya."
RSF bado haijatoa maelezo yoyote kuhusu tukio hilo.
Sudan imekuwa katika mgogoro mbaya kati ya Jeshi la Sudan na RSF tangu katikati ya Aprili 2023.
Mgogoro huo mbaya umesababisha vifo vya watu zaidi ya 27,120 na kusababisha watu milioni 14 kulazimika kukimbia makazi yao, na kuwa wakimbizi ndani au nje ya Sudan, makadirio ya mashirika ya kimataifa yanaonesha.
Watu wakiwa wamekusanyika karibu na miili ya watu waliofariki katika shambulio la vikosi vya wanamgambo Mjini Omdurman, Sudan, Desemba. 10, 2024. (Ofisi ya Habari ya Serikali ya Sudan ya Khartoum/kupitia Xinhua)
Watu wakiwa wamekusanyika karibu na basi la abiria lililobomolewa katika shambulio la vikosi vya wanamgambo Mjini Omdurman, Sudan, Desemba. 10, 2024. (Ofisi ya Habari ya Serikali ya Sudan ya Khartoum/kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma