Eneo la kumbukumbu ya TAZARA lazinduliwa nchini Zambia ili kuheshimu mchango wa Wachina waliojitolea

(CRI Online) Desemba 11, 2024

Hafla ya uzinduzi rasmi wa Eneo la Kumbukumbu ya TAZARA, lililojengwa kwa ajili ya kuwaenzi raia wa China waliopoteza maisha wakati wa ujenzi wa njia ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), imefanyika Jumanne katika Wilaya ya Chongwe, mashariki mwa Lusaka, nchini Zambia.

Hafla hiyo imewakutanisha pamoja maafisa wa serikali ya Zambia na wawakilishi kutoka Ubalozi wa China nchini Zambia na Shirika la Uhandisi wa Ujenzi la China (CCECC), kampuni inayohusika na ujenzi wa njia ya reli na eneo hilo la kumbukumbu.

Wang Sheng, Konsuli katika Ubalozi wa China nchini Zambia, amesema ufunguzi wa eneo hilo la kumbukumbu umekuja katika wakati mwafaka zaidi, kwani unasaidia kuendeleza ari ya TAZARA kwa vizazi vijavyo.

Amesisitiza kuwa ni wakati sasa kwa watu wa nchi zote mbili kuelewa vyema urithi wao wa pamoja na kushirikiana kwa ajili ya mustakabali wa pamoja, akibainisha kuwa wafanyakazi zaidi ya 60 wa China walipoteza maisha, 36 kati yao walizikwa Zambia.

Naye katibu mkuu katika Wizara ya Utalii ya Zambia, Evans Muhanga, amelielezea eneo hilo la kumbukumbu kuwa ni ushuhuda wa historia ya pamoja na dhamira ya nchi hizo mbili na watu wao.

(Picha inatoka tovuti ya Ubalozi wa China nchini Zambia.)

(Picha inatoka tovuti ya Ubalozi wa China nchini Zambia.)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha