

Lugha Nyingine
Madaktari wa China na Tanzania washirikiana kudhibiti ugonjwa wa Kichocho Kisiwani Pemba ili kulinda afya ya watu
Mtaalam wa kundi la wataalamu wa Mradi wa China wa Msaada wa Kudhibiti Ugonjwa wa Kichocho Zanzibar akitoa huduma katika shule kisiwani Pemba, akisambaza vipeperushi vya elimu kuhusu udhibiti wa ugonjwa wa kichocho. (Picha na Hu Zexin)
Watoto wa Kisiwa cha Pemba. (Picha na Gongming)
Wang Xinyao (kulia), mtaalam wa kundi la wataalamu wa mradi wa China wa msaada wa kudhibiti ugonjwa wa kichocho Zanzibar, akishiriki shughuli ya kupuliza dawa za kuua vimelea vya kichocho katika kisiwa cha Pemba, Zanzibar. (Picha na Wang Guanlin/Xinhua)
Kisiwa cha Pemba katika Visiwa vya Zanzibar nchini Tanzania hapo awali kilikuwa eneo lililoathiriwa zaidi na ugonjwa wa kichocho. Kwa sasa, hali hiyo inabadilika kutokana na juhudi za kundi la wataalamu wa mradi wa China wa msaada wa kudhibiti ugonjwa wa kichocho visiwani Zanzibar.
Bwawa moja katika Kata ya Kilindi, kisiwani Pemba ndicho chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wenyeji zaidi ya 4000. Wakiwa ni wabeba vimelea vyenye kueneza kichocho, Konokono wa malengelenge, huzaliana kwa wingi kwenye mabwawa kama hayo, na wakazi wanaoishi kando ya bwawa hilo huathirika sana.
“Tulishapuliza dawa za kuua konokono kwenye bwawa hili hapo awali, lakini sasa konokono hao wamejitokeza tena,” amesema Wu Hongchu, mtaalam wa kundi hilo la wataalamu wa China.
“Matumizi ya dawa za kuua konokono si suluhisho la kudumu. Ni kupitia tu kudhibiti na kuzuia kikamilifu, kubadilisha mazingira ya kuishi konokono, kubadili tabia za watu za matumizi ya maji, na kujenga ufahamu wa kuzuia ugonjwa, ndipo tunaweza kuondoa hatari fiche za maambukizi ya kichocho kutoka kwenye chanzo.”
Kisiwa cha Pemba kina jumuiya za makazi zaidi ya 120, mabwawa zaidi ya 300, na vijito zaidi ya 400. Tangu mradi huo wa China wa msaada wa kudhibiti ugonjwa wa kichocho ulipoanza rasmi mwaka 2017, Taasisi ya Utafiti wa Kuzuia na Kudhibiti Ugonjwa wa Kichocho ya Jiangsu imetuma wataalamu 40 kufanya kazi kwenye mradi husika.
Kuanzia uchunguzi na utembeleaji wa kina wa jumuiya za makazi hadi upimaji na matibabu ya ugonjwa ya nyumba kwa nyumba, kuanzia kwenda chini kwenye bwawa kuchunguza na kuteketeza konokono hadi kwenda kwenye kampasi za shule kufanya uenezi na kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo, nyayo za wataalamu hao wa China ziko kila kona ya kisiwa hicho.
Saleh Juma, msimamizi wa ofisi ya udhibiti wa magonjwa ya kitropiki kisiwani Pemba, amekuwa ukienda chini kwenye mabwawa hayo na kwenye jumuiya za wakazi na wataalamu hao wa China, na kuanzisha urafiki mkubwa nao. “Utafiti na mbinu za wataalamu wa China katika kudhibiti ugonjwa wa kichocho zimenihamasisha sana. Kujitoa kwao sana kwa kazi bila woga wa mambo magumu, kumehamasisha watu wengi wa Zanzibar kujiunga na juhudi hizi za kudhibiti kichocho,” amesema Sele.
Mwaka 2019, takwimu za tathmini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu awamu ya kwanza ya mradi huo zilionyesha kuwa, chini ya juhudi za pamoja za wataalamu wa China na wafanyakazi wenyeji, kiwango cha maambukizi ya kichocho katika eneo la kielelezo kisiwani Pemba kilikuwa kimeshuka kutoka asilimia 8.92 hadi asilimia 0.64.
Mwaka 2023, awamu ya pili ya mradi wa China wa msaada wa kudhibiti ugonjwa wa kichocho Zanzibar ilizinduliwa. Kwa kuzingatia mafanikio ya awamu ya kwanza ya mradi huo, awamu ya pili inalenga kupanua eneo hilo kielelezo la kudhibiti ugonjwa huo kisiwani Pemba na kuanzisha eneo la majaribio ya kudhibiti ugonjwa huo Unguja, kisiwa kikuu cha Zanzibar, ili kuhakiki na kusambaza zaidi mbinu zinazofaa za udhibiti wa kichocho kulingana na hali ya eneo husika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma