Rais Tshisekedi: DRC kuwa kitovu cha ubunifu kwa kituo cha utamaduni kilichofadhiliwa na China

(CRI Online) Desemba 12, 2024

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) itakuwa "kitovu cha kikanda cha ubunifu" kwa uzinduzi ujao wa Kituo cha Utamaduni na Sanaa cha Afrika ya Kati kilichofadhiliwa na China.

Hayo yamesemwa Jumatano na Rais Felix Tshisekedi wakati akilihutubia taifa mbele ya mabaraza mawili ya bunge la nchi hiyo.

Kituo hicho, ambacho jiwe lake la msingi liliwekwa na Tshisekedi mwaka 2019, “kitakuwa ni mahali maalum kwa ajili ya kuwasilisha sanaa, mafunzo, uvumbuzi na mabadilishano baina ya wabunifu” kutoka kwenye kanda na bara zima la Afrika, amesema.

Kituo hicho kina jumba kubwa la maonesho lenye uwezo wa kuchukua watu 2,000 wakiwa wamekaa kwenye viti na ukumbi mdogo wenye kuchukua watu 800. Pia kitakuwa makao ya kampasi mpya ya Taasisi ya Sanaa ya Taifa ya DRC, ambayo ni maarufu kwa kutoa mafunzo kwa vizazi vya wanamuziki na wasanii wa DRC.

Rais Tshisekedi pia alitaja miradi mingine ya miundombinu iliyojengwa na kampuni za China, ikiwemo barabara za mzunguko wa pete mjini Kinshasa. Baada ya kukamilika, miradi hiyo inatarajiwa kuimarisha muunganisho wa miundombinu kote nchini DRC.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha