

Lugha Nyingine
Kiwango cha kushughulikia makontena cha Bandari ya Shanghai, China chafikia milioni 50 kwa mwaka
Picha ikionyesha mandhari ya Gati la Yangshan la Bandari ya Shanghai, mashariki mwa China, Desemba 18, 2024. (Xinhua/Fang Zhe)
SHANGHAI - Bandari ya Shanghai imekuwa ya kwanza duniani kushuhudia uwezo wa kushughulikia makontena zaidi milioni 50 yenye urefu wa futi 20 (TEUs) kila mwaka jana Jumapili ambapo bandari hiyo imechukua nafasi hiyo ya kwanza kimataifa kwa miaka 14 mfululizo kwa uwezo huo.
Kwa mujibu wa Yang Yanbin, naibu meneja mkuu wa idara ya uzalishaji na biashara ya Kampuni ya Bandari ya Shanghai (SIPG), ukuaji huo wa uwezo wa kushughulikia makontena unaonyesha kuwa mfumo mzuri wa viwanda na uwezo wa uzalishaji bidhaa wa China unaendelea kuwezesha biashara ya kimataifa.
Ikiwa kama dirisha la kufungua mlango na ushirikiano, pia ni injini ya kukuza biashara na mawasiliano kati ya China na nchi za nje, Bandari hiyo ya Shanghai ilifikia kiwango cha kushughulikia makontena milioni 1 mwaka 1994.
Yang amesema kuwa ukuaji huo wa kushughulikia makontena katika Bandari ya Shanghai umetokana siyo tu na kuongezeka kwa makontena mazito ya kuuza bidhaa nje lakini pia na ongezeko la kiasi cha makontena ya kimataifa yanayopita na yale yanayohamishwa meli kwa meli.
"Uwezo mkubwa wa bandari na huduma bora zimevutia meli kubwa za mizigo kutoka duniani kote," amesema, akiongeza kuwa kiasi cha makontena yanayohamishwa meli kwa meli bandarini kinatarajiwa kufikia rekodi ya asilimia 60 mwaka 2024, ambayo inaonyesha kuimarika kwa nafasi ya Bandari hiyo ya Shanghai ya kuwa kitovu cha kimataifa.
Kwa sasa, Bandari hiyo ya Shanghai ina njia karibu 350 za meli za kimataifa zinazofikia bandari zaidi ya 700 katika nchi na maeneo zaidi ya 200 duniani kote.
Kwa mujibu wa Idara ya Forodha ya Shanghai, thamani ya bidhaa zinazoshughulikiwa na Bandari hiyo kwa kila siku ni wastani wa yuan bilioni 29.8 (dola za Kimarekani kama bilioni 4), ambayo ni yuan takriban bilioni 1.24 kwa saa.
Katika miaka ya hivi karibuni matumizi ya sayansi na teknolojia yameboresha sana ufanisi wa shughuli za magati kwenye bandari hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma