Qatar yafungua ubalozi tena mjini Damascus baada ya kufungwa kwa miaka 13

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 23, 2024
Qatar yafungua ubalozi tena mjini Damascus baada ya kufungwa kwa miaka 13
Bendera ya taifa ya Qatar ikionekana kwenye ubalozi wa Qatar mjini Damascus, Syria, Desemba 21, 2024. (Picha na Monsef Memari/Xinhua)

DAMASCUS - Qatar imefungua rasmi ubalozi wake katika mji mkuu wa Syria, Damascus siku ya Jumamosi, ikipandisha bendera ya taifa yake juu ya jengo hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 13 iliyopita.

Katika eneo la Abu Rummaneh mjini Damascus, wafanyakazi walikuwa wakisafisha eneo la ubalozi huo na kuondoa graffiti kutoka kwenye kuta zake.

Kufunguliwa tena kwa ubalozi huo kunakuja huku kukiwa na wimbi la wawakilishi wa kikanda na nchi za Magharibi wanaotembelea Syria kukutana na uongozi mpya wa nchi hiyo baada ya kuanguka kwa serikali ya aliyekuwa Rais wa Syria Bashar al-Assad mnamo Desemba. 8.

Pia inakuja karibu wiki moja baada ya ujumbe wa Qatar kutembelea Damascus kujiandaa kwa ajili ya kurejesha ujumbe wa kidiplomasia wa Qatar, ambao ulifungwa mwaka 2011 kufuatia kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Majed Al Ansari amesema wajumbe hao wamekutana na wawakilishi wa serikali ya mpito ya Syria na kusisitiza dhamira ya Qatar ya kusaidia watu wa Syria katika harakati zao za kutafuta usalama, amani, maendeleo na ustawi.

Mkutano huo pia ulijadili njia za kuimarisha kufikishwa kwa misaada ya kibinadamu ya Qatar nchini Syria na kutathmini mahitaji ya dharura ya wakazi wa Syria katika kipindi hiki muhimu, Al Ansari alisema.

Qatar ni nchi ya pili, baada ya Uturuki, kurejesha rasmi shughuli za kidiplomasia katika mji mkuu huo wa Syria tangu kuanguka kwa Assad.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha